WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso ameendelea kuwasha moto kwa Mameneja wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira (RUWASA), Mkoa wa Morogoro, baada ya kuamuru wengine wawili kurejeshwa wizarani kutokana na kushindwa kusimamia kwa weledi utekelezaji wa miradi ya maji vijijini.

Aweso amelazimika kuwarudisha wizarani Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Morogoro, Mhandisi John Msengi pamoja na Meneja wa Wilaya ya Kilombero, Mhandisi  Florence Mlelwa kutokana na kushindwa kwao kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji.

Akiwa wilaya ya Kilosa,  Waziri Aweso aliagiza Ruwasa Makao makuu kumpangia kazi nyingine Mhandisi  Joshi Chum, baada ya kutoridhishwa na utendaji kazi wake katika kusimamia miradi ya maji Kata ya Ruaha, mji mdogo wa Mikumi.

Waziri Aweso ametoa  uamuzi huo  Januari 6, 2023 kwenye  mkutano wa hadhara mji wa Mlimba Wilaya ya Kilombero, baada ya  kutoridhishwa na majibu ya Wahandisi wa Ruwasa Wilaya ya Kilombero pamoja na wa mkoa huo juu ya  utekelezaji wa mradi wa maji Kata ya Kalengakero.

Mradi wa maji katika kata hiyo umetengewa Sh milioni  282 pamoja na mradi wa maji wa Mji wa Mlimba uliotengewa Sh Milioni 600.

Waziri Aweso pia amevunja  Bodi ya Maji Mlimba na kuagiza kuundwa kwa mamlaka ya maji Mlimba, ambayo itakuwa na uwezo wa kuwahudumia wananchi wa mji huo, ambao ni makao makuu ya halmashauri ya Mlimba.

“ Haiwezekani nitoke wizarani nije kutatua changamoto za maji za watu wa Morogoro, wakati mamlaka husika zipo, lazima kila mtu awajibike kwa nafasi yake, huwezi huna budi kutupisha tuweke watu wengine wenye kuwajibika zaidi, ”amesema  Aweso.

Waziri Aweso alishangazwa na Meneja Ruwasa Wilaya ya Kilombero kushindwa kutumia Sh milioni 600, ambazo serikali imezitoa miezi kadhaa iliyopita kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji wilayani humo, ili kuondoa kero ya maji kwa wananchi na kutekeleza agizo la Rais la kumtua mama ndoo kichwani.

“Kama fedha hizo zingetumika ilivyokusudiwa, sasa hivi mama zangu na dada zangu msingekuwa mkipiga kelele, bali mngeutumia muda wenu vizuri, badala ya kutoka usiku kutafuta majii,” amesema  Aweso

Share To:

Post A Comment: