Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia masuala la Udhibiti Ubora wa Mazao ya Uvuvi na Masoko, kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Bw. Steven Lukanga akizungumza katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wachakataji wa mazao ya uvuvi Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma (kulia ) ni Afisa Mtaalam Mnyororo wa  Thamani wa Uvuvi na Ufugaji Viumbe Maji  Hashim Muumin.

Na Devotha Songorwa, Kigoma

WACHAKATAJI wa mazao ya uvuvi nchini wametakiwa kutumia fursa ya teknolojia katika shughuli zao ili kuboresha mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi na kukabiliana na upotevu wa mazao hayo katika Ziwa Tanganyika.

Hayo yamesemwa na Afisa Mtaalam Mnyororo wa  Thamani wa Uvuvi na Ufugaji Viumbe Maji  Hashim Muumin  wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wachakataji, wavuvi na  wafanyabiashara yaliyoandaliwa na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kupitia miradi yake ya  FISH4ACP  na Flexible Multi-partner Mechanism (FMM) mafunzo  ambayo yamefanyika mkoani Kigoma.

Afisa huyo alisema mradi wa FISH4ACP unatekelezwa katika nchi 12 za Africa, Caribbean na Pacific ambapo nchini Tanzania unafanyika katika Mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma ukilenga kukabiliana na changamoto  za upotevu wa mazao ya samaki kabla na baada ya shughuli za uvuvi, wakati wa uchakataji wa samaki na wakati wa kusafirishwa kwenda kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi.

“Mafunzo haya yamefanyika kwa njia ya filamu zilizonakiliwa kutoka Kenya, Uganda na Ghana lengo ni kuwawezesha wachakataji kujifunza njia bora za kuchakata mazao yao kama tulivyoona  kwa wenzetu wanatumia majiko banifu, chanja rafiki na salama za kuanikia dagaa,”alisema.

Pia ameongeza kuwa kupitia miradi hiyo wanatarajia kujenga miundo mbinu  ya kuchakatia dagaa na samaki  itakayoendana na mabadiliko ya tabia Nchi ambapo kwa sasa hatua zilizochukuliwa ni ufuatiliaji wa maeneo sahihi ya kuchakatia.

“Kama mradi tutatengeneza majiko ya kubanikia samaki tupate bidhaa nzuri kutoka Ziwa Tanganyika na tutaendelea na ufuatiliaji kuona kama mafunzo haya yanatafanya kazi kama tulivyokusudia na yatasaidia changamoto iliyopo sasa ya mabadiliko ya  tabianchi ,” alieleza.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia masuala la Udhibiti Ubora wa Mazao ya Uvuvi na Masoko, kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Bw. Steven Lukanga alibainsiha kuwa sekta ya uvuvi inachangia karibu asilimia 1.8 ya pato la Taifa wakati ulaji ukichangia asilimi 30 ya virutubishi vitokanavyo na wanyama.

“Ulaji wetu unaonekana tunakula wastani wa kilo 8. 5 badala ya kilo 20.5 kwa mwaka hivyo mafunzo haya yamekuja wakati muafaka yatasaidia kuboresha shughuli zetu tunazofanya hasa unapovua samaki wako au dagaa uhakikishe unawahifadhi sehemu salama na hata ukaushaji wetu uwe wenye manufaa kimasoko,” alifafanua.

Naye Afisa Uvuvi anayesimamia Wilaya ya Uvinza Bw. Venance Msongambele alisema elimu hiyo itawasaidia wadau wa uvuvi na wachakataji kuepuka kufanya kazi kwa mazoea,  na badala yake watakausha  samaki kwa kutumia mkaa  hatua inayoongeza thamani ya mazao hayo na kuvutia wateja.

“Kuna maboresho ambayo yakifanyika  yatatusaidia sana kama kupata barafu kuhifadhi samaki na dagaa, majiko ya mkaa  kwa sababu kuni siyo salama kwa afya kutokana na moshi  na kupitia mafunzo haya tumejifunza kufanya uchakataji kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira,”alieleza afisa huyo.

Akitoa shukrani zake Mchakataji kutoka Mwalo wa Katonga mkoani Kigoma Selestina  Silvester ameipongeza FAO kwa kuandaa semina hiyo kwani itawasaidia katika uhifadhi wa rasilimali za Ziwa Tanganyika kwa manufaa yao na Nchi kwa ujumla.

“Tunaishukuru sana FAO kwa kutoa  na elimu hii  inatusogeza kutoka hapa tulipo hadi sehemu nyingine  kwa sasa uchakataji tunafanya kienyeji sasa unakuta samaki au dagaa wanaharibika haraka kabla ya kufika sokoni na wanapungua ubora,”alisema Selestina. Afisa Mtaalam Mnyororo wa  Thamani wa Uvuvi na Ufugaji Viumbe Maji  Hashim Muumin.

Aidha Mwenyekiti wa Vyama vya Wavuvi Mkoa wa Kigoma Bwa. Francis John aliwahimiza wadau hao kutumia ujio wa mradi huo kama fursa muhimu kwao kuongeza thamani ya bidhaa zao ili kuendana na hali ya soko la sasa.

Baadhi ya wadau wa sekta ya uvuvi wakifuatilia mafunzo hayo kutoka kwa wawezeshaji (hawapo pichani).

Picha ya pamoja baada ya mafunzo hayo.

Afisa Mtaalam Mnyororo wa  Thamani wa Uvuvi na Ufugaji Viumbe Maji  Hashim Muumin akifafanua jambo wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wachakataji wa mazao ya uvuvi mkoani Kigoma.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: