Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Muhamed Mussa (wa pili kulia) akikata utepe kuzindua rasmi Mpango wa ufadhili wa masomo ya kuendeleza ujuzi kwa vijana kutoka kaya maskini na wanaoishi katika mazingira magumuWaziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar na Mgeni Rasmi Mhe. Lela Muhamed Mussa, akiongea kabla ya uzinduzi Mpango wa ufadhili wa masomo ya kuendeleza ujuzi kwa vijana kutoka kaya maskini na wanaoishi katika mazingira magumu.Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Muhamed Mussa ambaye ni Mgeni Rasmi pamoja na Mkurugezi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bi. Bahati Geuzye wakifuatilia salaam kutoka kwa viongozi mbalimbali waliohudhuria uzinduzi wa Mpango wa ufadhili wa masomo ya kuendeleza ujuzi kwa vijana kutoka kaya maskini na wanaoishi katika mazingira magumu.Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Bw. Khamis Abdulla Said akitoa neno la Ufunguzi katika hafla ya uzinduzi wa Mpango wa ufadhili wa masomo ya kuendeleza ujuzi kwa vijana kutoka kaya maskini na wanaoishi katika mazingira magumu iliyofanyika Desemba 14, 2022 ZanzibarLela Muhamed Mussa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar (Wa pili kushoto) ambaye ni Mgeni Rasmi akisikiliza kwa makini taarifa kutoka kwa wanafunzi wa fani ya huduma za ukarimu ambao wanasoma kupitia Mpango wa ufadhili wa masomo ya kuendeleza ujuzi kwa vijana kutoka kaya maskini na wanaoishi katika mazingira magumu. Kulia kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Bw. Khamis Abdulla Said, kutoka kushoto ni mjumbe wa Bodi ya TEA Bi. Mystica Mapunda, Mkurugenzi Mkuu wa TEA Bi. Bahati Geuzye na Mwenyekiti wa Bodi ya TEA Prof. Maurice Mbago Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) akizungimza katika hafla ya uzinduzi wa Mpango wa ufadhili wa masomo ya kuendeleza ujuzi kwa vijana kutoka kaya maskini na wanaoishi katika mazingira magumu Zanzibar

********************

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mhe. Lela Mohamed Mussa leo tarehe 14 Desemba 2022 amezindua Mpango wa Ufadhili wa Mafunzo ya Kuendeleza Ujuzi kwa Vijana kutoka Makundi Maalumu na Wanaoishi Katika Mazingira Magumu (Bursary Scheme for Vulnerable Groups) katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST).

Mpango huu wa Ufadhili unasimamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) chini ya Programu ya Kukuza Ujuzi na Stadi za Kazi kwa ajili ya ajira zenye Tija (Education and Skills for Productive Jobs-ESPJ) unaoratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. SDF inafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia na jumla ya vijana 600 watanufaika kutoka Zanzibar.

Mhe. Lela amesema, lengo la ufadhili wa mafunzo ya ujuzi unaotolewa ni kuwezesha vijana wa kitanzania wanaotoka katika makundi maalum na kaya maskini kupata ujuzi na stadi za kazi zitakazowawezesha aidha kuajiriwa au kujiajiri wao wenyewe hivyo kuchangia jitihada za Serikali za kuwawezesha wananchi wake wa makundi yote ki-uchumi na kijamii.

Aidha Mhe. Lela amesema anaona fahari kushiriki katika hafla ya uzinduzi wa Mpango huo wa mafunzo ya ujuzi kwa ajili ya vijana 600 ambao watapata fursa ya kupatiwa mafunzo ya ujuzi katika fani za ushonaji, umeme wa majumbani, udereva, useremala, ufundi bomba, ujenzi, ufundi magari, uchomeleaji, ususi na urembo, upishi, kompyuta, utengenezaji majokofu na kilimo bustani.

Amesisitiza kwamba, mafunzo hayo yanaenda sanjali na programu ndogo ya Mafunzo ya Amali ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kama ilivyoanishwa kwenye Bajeti ya Wizara hiyo ya mwaka 2022/ 2023 ya kutoa elimu itakayowawezesha vijana kujiajiri ili kujikwamua na umasikini.

TEA imepewa jukumu la kusimamia na kutekeleza Mpango huu na Wizara mama ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa lengo la kuwafikia vijana kutoka makundi maalumu na wanaoishi katika mazingira magumu walio katika kaya zilizosajiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuhakikisha wanafaidika na mpango huu kwa kuwapatia ujuzi utakaowawezesha kujikwamua ki-uchumi.

Mwenyekiti wa Bodi ya TEA Prof. Maurice Mbago ni mmoja kati ya viongozi waliohudhuria hafla hiyo ya uzinduzi ambapo amesema, TEA ilipewa jukumu la kuratibu utekelezaji wa Mfuko wa SDF mwaka 2017 na awamu ya kwanza ya utekelezaji ilifanyika mwaka wa fedha wa 2017/2018 huku awamu ya pili ambayo inaendelea yenyewe ilizinduliwa rasmi mwaka 2020.

Prof. Mbago ameweka bayana kuwa, TEA kwa kushirikiana na Benki ya Dunia imekamilisha taarifa ya ufuatiliaji wa wanufaika (Tracer Study) kwa lengo la kupima matokeo ya mafunzo ya kuendeleza ujuzi kwa wanufaika waliopata nafasi kushiriki mafunzo hayo. Ufuatiliaji huo uliohusisha wanufaika 3,871 kati ya wanufaika zaidi ya elfu 35,000, umeonyesha kuwa asilimia 81 ya wanufaika hao wameajiriwa au wamejiajiri ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tangu walipopata mafunzo ya ujuzi.

Nae Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania Bi. Bahati Geuzye amefafanua kwamba, Mpango huu unatoa ufadhili wa mafunzo ya ujuzi katika sekta sita za kipaumbele ambazo ni: Kilimo na Kilimo - biashara, Utalii na huduma za Ukarimu, Uchukuzi, Ujenzi, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na Nishati. Mpaka sasa vijana wa kitanzania takribani 35,000 wamenufaika na mafunzo ya ujuzi tangu yalipoanza kutekelezwa mwaka 2018 ambapo kiasi cha Sh. Bil 13. 8 zimeishatumika ikiwa ni fedha zilizoelekezwa moja kwa moja kwa Taasisi 143 za Mafunzo ili kuwezesha mafunzo.

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ni Taasisi ya Umma inayofanya kazi chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. TEA inaratibu Mfuko wa Elimu wa Taifa ambao unasaidia jitihada za Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu kwa lengo la kuongeza ubora wa elimu na upatikanaji wake kwa usawa. Pia TEA inaratibu Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: