Denisi Chambi, Tanga. 

Halmashauri ya jiji la Tanga kwa mwaka ujao wa masomo 2023 imelenga kuwaandikisha wanafunzi 6400 kwa ngazi ya awali mpaka sasa wakiwa tayari wamefikia asilimia 48 % huku kwa upande wa darasa la kwanza wakilenga kuwaandikisha wanafunzi 9400 ambapo tayari wameshafikia asilimia 62% pekee. 

Hayo yamebainishwa na mstahiki meya wa halmashauri hiyo Abdurahman Shillow wakati akiwahamasisha wazazi na walezi kuhusiana na zoezi hilo kupitia vyombo vya habari ofisini kwake ambapo amesema kuwa bado malengo hayajafikiwa na mwisho wa uandikishaji ikiwa ni December 30, mwaka huu.

 "Niwasihi na kuwaomba sana wazazi na walezi wa jiji hili la Tanga kwamba uandikishaji wa watoto katika madarasa yetu ya awali utamalizika tarehe 30, December, lakini pia uandikishaji wa watoto wetu wa darasa la kwanza utamalizika rasmi tarehe hiyo hiyo, niwaombe sana wazazi wote wenye watoto wa kiume na wakike, wenye ulemavu na wasio na ulemavu shule ziko wazi na walimu wapo kwaajili ya shughuli za uandikishaji" alisema Shillow.

 "Mpaka sasa tathmini zinaonyesha katika elimu ya awali tumefanya uandikishaji kwa asilimia 48% katika asilimia 100% tulitegemea tuandikishe watoto zaidi ya 6400 lakini mpaka sasa hivi tumeandikisha watoto 3200 tu maana yake kuna watoto zaidi ya 3000 bado hawajaandikishwa kwahiyo tunawasisitiza wazazi na walezi wa watoto wa madarasa ya awali twende tukaandikishe watoto wetu" 

"Lakini kwa elimu ya darasa la kwanza tulitarajia tuandikishe watoto 9400 mpaka sasa tumeandikisha watoto 5800 maana yake tumeandikisha asilimia watoto 62 % zaidi ya asilimia 38% hatujaandikisha kwahiyo tunaomba wazazi wito huu muupokee kwa haraka kwa siku hizi chache zilizobaki mukawapeleke watoto kwa maslahi mapana ya watoto wetu , mji wetu na jamii ya watu wa Tanga kwa ujumla" alisema Mstahiki Meya.

 Aidha Shillow amewasisitiza wazazi na walezi kuhakikisha wanaungana kwa pamoja na kamati za shule , kamati za maendeleo za kata na mitaa kujitolea na kuwa tayari katika kuchangia chakula kwaajili ya wanafunzi hasa waliopo madarasa ya awali na darasa la kwanza hii ikilenga hasa kuhakikisha wanainua kiwango cha uelewa na ufaulu kwa wanafunzi wakati wanapokuwa mashuleni sambamba na kupambana na utoro. 

"Elimu ili iwe bora lazima iende sambamba na swala zima la lishe hususani kwa wanafunzi wetu wa madarasa ya awali , watoto hawa hawana uwezo wa kuvumilia kukaa bila kula kwahiyo niwaombe wazazi na walezi kupitia kamati zao za shule , kamati zao za maendeleo za kata na mitaa wajitolee kuchangia lishe kwa sababu ni swala linalomhusu mtoto moja kwa moja na elimu bora itapatikana mtoto atakapokuwa ameshiba vizuri" 

Hata hivyo aliongeza kuwa mpaka sasa hali ya miundombinu iko shwari kila sehemu ambapo jiji hilo limejipanga kuhakikisha kuwa shule zote 81 kwa mwaka 2023 watoto wote wanakuwa katika mazingira safi, salama na rafiki kwaajili ya kujifunzia.

"Miundombinu ya madarasa , madawati vyoo na miundombinu ya walimu imejitosheleza kwa asilimia kubwa kwahiyo hakuna mtoto atakayekaa chini na watakaa kwenye madawati shule zote 81 zimejitosheleza sasa hivi halmashauri tumejipanga niwasisitize tu wazazi watumie fursa na kuwapa watoto haki yao ya kusoma" aliongeza 

Aidha mstahiki meya amewataka wenyeviti wa mitaa pamoja na watendaji wote wahakikishe kuwa hakuna mtoto ambaye anabaki nyumbani wakati anapaswa kuwepo shuleni akiwataka kuwaelimisha wazazi na walezi juu ya umuhimu wa elimu lakini pia kuwachukulia hatua za kisheria wale watakaokaidi ama kupuuzia suala la elimu kwa watoto.

 "Niwaombe sana wenyeviti wa serikali za mitaa na watendaji wote wa serikali za mitaa waelewe kwamba elimu ni haki ya mtoto kwahiyo tukiwa kama viongozi kwenye mitaa tunapaswa kuhakikisha kila mtoto anapata haki yake hiyo kwa kuwapa elimu wazazi na walezi lakini pale inapoonekana elimu imetolewa na watu hawataki kutekeleza basi sheria ichukue mkondo wake"
Share To:

Post A Comment: