Na Denis Chambi, Tanga.

 Jeshi la Polisi mkoa wa Tanga limefanikiwa kumkamata mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Zainabu Kagoso mkazi wa Dar es salaam mwenye umri wa miaka 50 aliyekuwa akijitambulisha kuwa ni mshauri wa rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan  katika mambo ya kijeshi na kutumia njia hiyo kutapeli katika ofisi za serikali na maeneo mbalimbali wilayani Kilindi. 

Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari ofisini kwake kamanda wa jeshi la Polisi mkoa wa Tanga Henry Mwaibambe amesema kuwa mtu huyo mara baada ya kukamatwa alidai kuwa ni afisa usalama yupo Tanga kwa kazi maalum ambapo amekuja kufwatilia kazi mbalimbali alizotumwa.

 "Katika opareshini zetu tumefanikiwa kumkamata mtu mmoja mwanamke ambaye ni mkazi wa Ukonga Dar es salaam amekuja mkoani Tanga hasa wilaya ya Kilindi akiwa anaenda ofisi mbalimbali za serikali akidai kwamba yeye ni afisa usalama wa Taifa na amekuja kwa kazi maalum na kwamba yeye ni mshauri wa rais Samia Suluhu Hassan katika mambo ya kijeshi amekuja kuangalia kazi mbalimbali aliyotumwa tulimfwatilia na tulifanikiwa kumkamata na tumemfikisha mahakamani jana (jumatatu) kwa kujifanya kuwa ni afisa wa serikali" alisema Kamanda Mwaibambe

 Aidha katika wilaya ya Lushoto watu wanne wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kujihusisha na mauaji ya ndugu yao aliyefahamika kwa jina la Ally Zayumba mwenye umri wa miaka 52 aliyeuwawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani hadi kupasuka ambapo awali taarifa zililipotiwa na ndugu zake katika kituo cha Polisi wilayani humo kuwa mtu huyo amepotea na baadaye mwili wake kupatikana ukiwa umetupwa.

 "Vile vile jeshi la polisi tumefanikiwa kuwakamata watu wanne na kuwafikisha mahakamani kwa tuhuma ya mauaji yaliyotokea November 14, 2022 katika kijiji cha Sunga wilaya ya Lushoto ambapo Ally Zayumba mwenye miaka 52 aliuwawa kwa kupigwa kitu kizito kichwani na kichwa kupasuka awali ndugu zake walilipoti kwenye kituo cha Polisi wakidai kuwa ndugu yao amepotea na hajulikani yuko wapi"

 "Upelelezi wa Polisi uliendelea tulimkamata mtu mmoja anaitwa Omary Issa( 25) ambaye ni ndugu wa Marehemu katika mahojiano alikiri kwamba yeye na ndugu zake wengine ndio wameshiriki katika mauaji ya huyo ndugu yao na walikuwa tayari kwenda kutuonyesha mahali walipotupa huo mwili, na kueleza kuwa sababu za mauaji hayo wana migogoro ya kifamiliya" alieleza 

Aidha katika taarifa nyingine kamanda mwaibamne amesema kuwa wilayani Handeni November 23 jeshi hilo limefanikiwa kumkamata Habibu Botela miaka 49 akiwa na meno manne ya Tembo akiyasafirisha kupitia pikipiki ambapo tayari ameshafikishwa mahakamani kutokana na kosa hilo linalomkabili.

 "Katika eneo kwa Kwediboma wilaya ya Handeni majira ya saa 7 mchana alikamatwa mtu mmoja Habibu Botela miaka 49 mkazi wa Kibirashi akiwa na meno manne ya Tembo aliyokuwa ameyahifadhi kwenye mfuko wa Salfeti na kusafirisha kupitia pikipiki yenye namba za usajiri T 273 DKT mtuhumiwa huyu ameshafikishwa mahakamani tayari" alisema kamanda huyo. 

Aliekeza kuwa jeshi la Polisi limeendelea na oparesheni mbalimbali za kupambana na uhalifu ambapo limefanikiwa kukamata Bhangi kilo 50.5, Mirungi kilo 87 wahamiaji haramu 9 , dumu 4 za mafuta ya kula pombe aina ya Gongo lita 95 pamoja na mitungi ya gesi 36.

 Katika kuelekea sikukuu za Krismas na mwaka Mpya kamanda Mwaibambe amewahakikishia wananchi wa mkoa wa Tanga kuwepo kwa hali nzuri ya ulinzi na usalama huku akiwatahadharisha kutokujihusisha na vitendo vyovyote vya uhalifu akisema kuwa jeshi la Polisi limejipanga kuwachukulia hatua kali za kisheria.

 "Kuelekea mwisho wa mwaka sikukuu za mwisho wa mwaka sio ngeni kwetu, jeshi la polisi limejipanga kuanzia usalama wa barabarani tuko kazini kukagua ili kuhakikisha kwamba watumiaji wa vyombo vya usafiri wanafuata sheria za barabarani, lakini ulinzi umeimarishwa maeneo yote muhimu yenye mikusanyiko ya watu , ombi letu kwa wananchi watupe ushirikiano wa kutoa taarifa yeyote ya mhalifu na wahalifu au dalili yeyote ya uvunjifu wa amani tunaomba watupe taarifa mapema" alisema kamanda Mwaibambe
Share To:

Post A Comment: