WAZIRI wa maji Jumaa Aweso, amewaagiza wakurugenzi wa mabonde ya mito kuhakikisha wanasimamia na kushirikiana na watendaji wa Taasisi nyingine kudhibiti uharibifu wa vyanzo vya maji ili mito iendelee kubaki salama .

Aidha amesema changamoto ya upungufu wa maji ni kipindi cha mpito hivyo kila mmoja kwa nafasi yake kuanzia ngazi ya jamii washirikiane kupambana na tatizo hilo ili kurejesha hali ya kawaida ya upatikanaji wa maji.

Akizungumza na viongozi mbalimbali mkoani Pwani, katika ukumbi wa mikutano wa mkuu wa mkoa wa Pwani ,Aweso alieleza Taasisi yoyote imara inapimwa kwa kipindi cha matatizo hivyo hakuna namna ya pekee ya kushinda vita hii zaidi ya kukubali ushirikiano.

"Nchi yetu ina mabonde tisa ,Wizara ya maji Ina wajibu wa kuyasimamia ,nimefanya ziara nchi nzima ,nimejifunza kuna mkurugenzi wa bonde ukimuuliza je anajua Raslimali za maji na mito lakini unakuta hazijui" Ni wajibu wetu kushirikiana pamoja watu wa bonde,TFS , watendaji wa maji, Mazingira kupata suluhu "

"Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine kuwa pamoja na Wizara ya maji katika kipindi hiki Cha mpito" Kwa hakika Rais wetu Samia Suluhu ni Suluhu ya matatizo ya Watanzania,alifafanua Aweso.

Hata hivyo Aweso alieleza ,maji ni muhimu ,na huduma ya maji haina mbadala ambapo kwa mujibu wa sensa Watanzania wapo milioni zaidi ya 61,ukikadiria mtanzania mmoja anatumia mita za ujazo wa maji 2,250 kwa mwaka wakati mwaka 1961 mtanzania mmoja alitumia mita za ujazo 12,000.

"Mwaka 1961 kulikuwa na takriban Watanzania milioni 10, maji ujazo wa milioni 126 ,kati yake Raslimali za maji zilizopatikana juu ya ardhi ilikuwa milioni 105 huku Raslimali za maji zilizopatikana chini ya ardhi ni mita za ujazo milioni 121 ,ukikadiria kwa mtanzania mmoja alikuwa anatumia ujazo 12,000 kwa mwaka."alibainisha Aweso.

Awali mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge, alitoa agizo kwa wakuu wa wilaya na kamati za ulinzi kuhakikisha wanazuia kuchepusha maji na kuzuia uharibifu wa mito inayopita kwenye Maeneo yao.

Agizo jingine , kuhakikisha mifugo inayotoka mikoa mingine haiingi mkoa wa Pwani na iliyoingia irudi ilipotoka.

Kunenge alielezea kwamba , wafugaji wasitumie nguvu kudhuru wananchi,kwani hakuna alie na nguvu zaidi ya mwingine na atakaejaribu kufanya hivyo atashughulikiwa .
Akizungumzia changamoto ya uharibifu wa mazingira, Kunenge alikemea ukataji miti ovyo sanjali na uchomaji mkaa holela.

Mwenyekiti wa bodi ya DAWASA Jenerali mstaafu Davis Mwamnyange alisema ,maji ndio tegemeo kubwa kwa binadamu, na maji hayana mbadala ,lazima vyanzo vya maji vitunzwe ili DAWASA iweze kutimiza wajibu wao wa kuhakikisha huduma ya maji inapatikana.
Share To:

Post A Comment: