Halmashauri Kuu ya CCM chini ya mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan ilimaliza kikao chake jijini Dodoma jana kuchuja majina ya viongozi wa ngazi ya mkoa ukiwa ni mtihani wa kwanza kwa Samia tangu ashike wadhifa huo Machi 19 mwaka jana.

Safu inayojengwa sasa itafanya maandalizi yote muhimu ya mpambano wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.


Hata hivyo, taarifa za ndani ya kikao hicho zinasema panga la Samia limewapitia zaidi ya wenyeviti 10 wa mkoa.

“Naomba utambue kuwa sura mpya nyingi zitaibuka maana wenyeviti 11 wamefyekwa miongoni mwao ni wa Mkoa wa Songwe, Mara na Iringa, kwa hiyo huko goli ni jeupe,” alisema mumbe aliyeomba kutotajwa.

Taarifa za uhakika zinataja utaratibu wa cheo kimoja kwa mtu mmoja huenda ikaachwa kwani baadhi ya waliopitishwa tayari wanayo majukumu mengine ndani ya chama hicho kwa mfano Mbunge wa Makambako, Deo Sanga aliyepitishwa kugombea uenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe.

Kipindi cha utawala wa hayati John Magufuli, CCM kilipiga marufuku kujilimbikizia vyeo na kutaka cheo kimoja kiwe kwa mtu mmoja.

Kabla ya kuwa mbunge, Sanga alikuwa diwani na wakati huohuo akawa mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa kabla ya kugawanywa kuipata Iringa na Njombe ambako aliongoza mkoa huo.

Kukatwa kwa majina kunakuja katika kipindi ambacho wenyeviti wengi wa wilaya walioomba kutetea nafasi zao walikatwa na wilaya hizo kuwa na wagombea wapya.

Wilaya nyingi majina yalikatwa na miongoni mwao ni Chamwino na Mpwapwa zote za Dodoma.

Mmoja wa wajumbe wanaomaliza muda wao alisema jana upitishwaji wa majina ya wagombea ulikuwa wa makini zaidi kwani chama kinaandaa watu wa kukivusha 2025 ambako chama kinajiandaa kushinda.


“Wengi waliingia kwa mhemuko na wengine walijenga makundi ambayo bila kuwa makini yanaweza kutukwamisha siku za usoni, mama kajitahidi na timu yake imempa ukweli,” alisema mjumbe huyo.


Kikao kilivyokuwa

Juzi, wajumbe waliingia mapema ndani ya ukumbi wa White House na ilipofika saa sita mchana taarifa zilianza kusambaa kuhusu waliokatwa na waliobakizwa kwani baadhi ya wajumbe walitoka na kukaa katika vikundi kipindi cha mapumziko.

Wakati wa kuingia wengine walisikika wakieleza namna kutakavyokuwa na mgawanyiko kwa madai ya kutoswa kwa wakongwe na kuchukuliwa wapya.

Waliogombea na majina yao kutajwa walikuwa ni Waziri wa Nishati, January Makamba, waliowahi kuwa mawaziri Alhaji Haji Mponda, Dk Mary Nagu, Balozi Philip Marmo, Sophia Simba na Dk Anthony Diallo.

Wengine ni waliowahi kuwa wakuu wa mkoa; Mecky Sadick, Henry Shekifu na Loata Sanare na waliowahi kuwa wakuu wa wilaya akiwamo Lembrice Kivuyo na Christopher Kangoye.

Pia wamo Mbunge Tarimba Abbas na Josephat Gwajima na mbunge wa zamani, James Lembeli na Adam Kimbisa aliyekuwa meya wa Dar es Salaam.


Jumuiya wapitishwa

Waliopitishwa kuwania uenyekiti wa Jumuiya ya Vijana (UVCCM) baada ya Kheri James kuteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Ubungo ni Farid Mohamed Haji, Kassim Haji Kassu, Mohamed Ali Momahed na Abdallah Ibrahim Natepe kutoka Zanzibar.

Watakaowania umakamu mwenyekiti ni Khadija Khalid Ismail, Dorice John Mgeta, Victoria Charles Mwanziva na Rehema Sombi Omary.

Uenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) unawaniwa na Gaudentia Kabaka anayetetea nafasi hiyo sawa na mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba akipambana na mbunge wa zamani wa Korogwe Vijijini, Mary Chatanda, Dk Wemael Chamshama na Mariam Lulida.


Nafasi ya makamu mwenyekiti UVCCM waliopitishwa ni Latifa Nasser Ahmed, Thuwaybah Kissasi, Hafsa Said Khamis na Zainab Khamis Shomari.

Katika Jumuiya ya Wazazi wamepitishwa wagombea tisa akiwemo Dk Edmund Mndolwa anayetetea nafasi hiyo, Fadhili Maganya, Bakari Kalembo, Said Mohamed, Mwanamanga Mwaduga, Ally Maulid Othuman, Ali Khamis Masudi na Hassan Haji Zahara huku umekamu ukiwaniwa na Haidar Haji Abdalla, Dk Wemael Chamshana, Fatma Abeid Haji, Rachel Kabunda, Neema Mturo, Zahoro Salehe Mohamed na Dogo Idd Mabrouk.


Chanzo : Mwananchi


Share To:

Post A Comment: