Na Elizabeth Joseph, Monduli.


MFUKO wa Maendeleo ya Jamii(TASAF) Wilaya ya Monduli umenufaika kupitia Ufadhili wa Umoja wa Nchi zinazosambaza mafuta Duniani(OPEC) kwa kuibua miradi mbalimbali kwa wananchi wilayani humo ili kupunguza umasikini.

Hayo yamesemwa na Mratibu wa TASAF Wilaya ya Monduli Bi,Lineth Chiduo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mpango katika mkutano wa Mkuu wa Wilaya hiyo pamoja na viongozi wa Dini na Wazee wa Mila.

Bi Chiduo alieleza kuwa utekelezaji wa miradi ya kupunguza umasikini Awamu ya kwanza na ya pili ulikuwa wenye mafanikio makubwa hivyo kuwavutia baadhi ya wadau wa maendeleo katika kuunga jitihada za serikali za kupunguza umasikini kwa kutekeleza miradi mbalimbali chini ya usimamizi wa TASAF.

"Moja ya wadau wanaounga mkono utekelezaji wa TASAF Awamu ya 3 ni Umoja wa Nchi zinazosambaza mafuta Duniani ( OPEC),Wilaya ya Monduli inanufaika na Ufadhili wa OPEC kwa Awamu ya 4 ambapo jumla ya miradi minne iliyoibuliwa katika vijiji vinne imepatiwa kiasi Cha shilingi Milioni 340,167,106.01 katika Awamu ya kwanza"alisema 

Alibainisha miradi hiyo kuwa ni pamoja na Ujenzi wa chumba cha upasuaji katika Zahanati ya Engaruka juu ambao umegharimu kiasi Cha shilingi Milioni 92,410,714.20  na imefikia hatua ya umaliziaji huku Engaruka ya Chini umejengwa mradi wa Maabara katika Zahanati ambayo umegharimu shilingi Milioni 84,559,303.21.

Aliongeza kusema miradi mingine mi ujenzi wa madarasa mawili,Ofisi ya walimu na unjezi wa Choo matundu sita katika Shule ya Msingi Migungani ambayo ipo katika hatua ya umaliziaji.

Aidha alisema kuwa katika Awamu ya pili Halmashauri hiyo ilipokea kiasi Cha shilingi Milioni 281,087,003 chini ya mpango wa kupunguza umasikini na OPEC Awamu ya 4 ambazo zimejenga nyumba ya Mwalimu wa Sekondari na Msingi Migungani B pamoja na nyumba ya Mwalimu wa Shule ya Msingi Mti mmoja na kuongeza nyumba zote ziko katika hatua ya umaliziaji.

Bi Chiduo alitaka mafanikio ya mpango huo katika kipindi Cha pili Cha utekelezaji kuwa ni pamoja na Kaya 4,367 kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya iliyoboreshwa(CHF) pamoja na vijiji vitano kunufaika na Ujenzi wa mabwawa sita yenye uwezo wa kuhifadhi Lita za ujazo 485,000 kwa matumizi ya binadamu na wanyama.

"Mpango wa OPEC umeweza kujenga madarasa matano,kuweka madawati 115,nyumba za walimu 8,bweni moja na vitanda vyake linalokaa wanafunzi 48,mabafu 10 na vyoo matundu 40"aliongeza.

Hata hivyo alitaja changamoto zilizopo katika kutekeleza mpango huo kuwa ni madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabia Nchi kuathiri utekelezaji wa baadhi ya miradi hasa katika ufugaji kwenye vikundi kwakuwa baadhi ya mifugo imeathirika na Ukame, magonjwa na hata kufa.

Aliongeza kutaja changamoto nyingine kuwa ni baadhi ya vijiji kuwa na miundombinu duni ya barabara na simu hivyo kuwa vigumu kufika kuhudumia walengwa hasa kipindi Cha mvua pamoja na tatizo la Mifumo ya fedha kuchelewa kufunguliwa hivyo kusababisha miradi kuchelewa kukamilika.


Share To:

Post A Comment: