Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Tanga   kamishina msaidizi mwandamizi Henry Mwaibambe  akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo November 11,2022.
                
NA DENIS CHAMBI, TANGA.
 
Jeshi la Polisi mkoa wa Tanga limefanikiwa kumkamata mtu mmoja mfanyabiashara Freddy Rujwauka mwenye umri wa miaka 67 ambaye pia ni mmiliki wa ukumbi BMK Sahare uliopo jijini kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya uhalifu wa aina tofauti tofauti katika mikoa ya Tanga na Dar es salaam. 

Akizungumza na waandishi wa habari kamanda wa jeshi la Polisi mkoa wa Tanga kamishina msaidizi mwandamizi Henry Mwaibambe amesema kuwa mtuhumiwa huyo aliyekuwa akijihusisha na makosa mbalimbali anatarajiwa kupelekwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika.

 "Tunamshikilia mtu mmoja mfanyabiashara na mmiliki wa ukumbi wa BMK Sahare kwa kosa la kujihusisha na vitendo vya uhalifu katika mikoa ya Dar es salaam na Tanga kwa sasa hivi tunaye ameletwa kutoka Dar es salaam na tunakamilisha taratibu ili mapema wiki ijayo afikishwe mahakamani " alisema Kamanda Mwaibambe. "

Kumekuwa na kelele nyingi kutoka kwa ndugu zake wakitumia mitandao ya kijamii wakidai kuwa mtu wao hajulikani yuko wapi kitu ambacho sio cha kweli alivyokuwa amekamatwa Dar es salaam ndugu zake walijulishwa na walikuwa wakimletea chakula na hata hapa Tanga walikuwa wakimletea chakula hivyo tunatarajia kumfikisha kwa makosa aliyokuwa akijihusisha nayo" aliongeza 

Aidha kamanda Mwaibambe amesema kuwa jeshi la Polisi linaendelea na oparesheni ya kubaini mtandao wa wahamiaji haramu ambapo hivi karibuni katika wilaya ya Handeni walifanikiwa kukamata wahamiaji haramu 38 wote wakiwa ni wanaume raia wa Ethiopia waliokuwa wakisafirishwa kwa njia ya gari wakiingia hapa nchini kupitia mpaka wa Tarakea mkoani Kilimanjaro wakitokea nchini Kenya. 

Alisema ameongeza kuwa mara baada ya mahojiani na wahamiaji hao walikiri kuwa wametoka nchini Ethiopia kuelekea nchini Afrika Kusini kutafuta maisha ambapo baadhi yao walikutwa na Paspoti za Ethiopia zenye mihuri ya Kenya.

 "Tunaendelea na kukamata mtandao wa wahamiaji haramu hasa watu ambao wanawapokea wahamiaji haramu kutoka nchi jirani ambapo mnamo tarehe 10-11-2022 katika wilaya Handeni mkoa wa Tanga walikamatwa raia 38 wa Ethiopia wote ni wanaume wakiwa wameingia nchini bila kibali na kinyume cha sheria"

 "Kati ya wahamiaji waliopekuliwa wawili walikutwa na paspoti za Kenya zinayoonyesha waliingia nchini Kenya kupitia mpaka wa Moyake na watuhumiwa wote wamekiri kuwa wametoka nchini Ethiopia kwenda nchini Afrika Kusini kutafuta maisha na wanaeleza kuwa baadhi yao paspoti zao zilichukuliwa na wakala wao ajulikanaye kwa jina moja la Martine raia wa kenya na ndiye aliyewatafutia usafiri" alisema Kamanda huyo. 

Kamishna msaidizi wa uhamiaji mkoa wa Tanga Kagimbo Hosea amesema miongoni mwa mpango mikakati iliyopo kwa sasa katika kuhakikisha wanadhibiti mianya yote inayotumika kupitisha wahamiji haramu ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na madhara ya kujihusisha na uhamiaji haramu ambapo wameanzisha kampeni ya 'Mtambue jirani yako' yenye lengo la kuwapatia wananchi elimu ili kutoa taarifa za mitandao yote ya uhamiaji haramu katika maeneo yao wanayoishi .

          Kamishna msaidizi wa uhamiaji mkoa wa Tanga Kagimbo Hosea akionyesha kwa waandishi wa habari  moja ya Paspoti zilizokamatwa kwa wahamiaji haramu  raia wa Ethiopia waliokamatwa hivi karibuni wilayani Handeni. 

 "Sisi kama idara ya uhamiaji kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama tumejipanga kutoa elimu kwa wananchi ili kuonyesha madhara ya uhamiaji haramu na tumeanza na kampeni ya mtambue jirani yako ukimjua jirani yako itasaidia kupunguza tatizo la uhamiji haramu hivyo ni vyema kuelimishana ili tatizo hili lipungue au likome kabisa na hii itatusaidia kwa kiasi kikubwa sana " alisema Hosea. 

Aidha amewataka wananchi kutokujihusisha na kusafirisha au kuhifadhi wahamijia haramu katika maeneo yao wanayoishi badala yake watoe taarifa kwenye vyombo vya dola ili kurahisisha jitihada mbalimbali zinazofanyika hapa nchini kupunguza au kuondokana kabisa na wimbi la wahamiji haramu wanaokuja nchini kinyume cha taratibu na sheria zilizopo.
Share To:

Post A Comment: