Na Gift Mongi,Moshi


Mpango ujao wa maendeleo 2023/2024  unaweza usikamilike kama wakulima hawataangaliwa kwa jicho la kipekee ili kukuza sekta hiyo muhimu ambayo ndio uti wa mgongo wa taifa letu.


 Kwa mantiki hiyo jambo  linalotakiwa kufanyika kwa sasa  ni kuhakikisha serikali inatenga fedha za kutosha katika pembejeo za kilimo ili kuwapatia wakulima mbegu, mbolea na viwatilifu ili uzalishaji uweze kukamilika.


Mbunge wa jimbo la Moshi Vijijini Prof Patrick Ndakidemi ametoa kauli hiyo Bungeni alipokuwa akichangia hoja katika sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambapo ameishukuru Serikali kuwekeza Bilioni 100 kwenye ruzuku za pembejeo za kilimo hasa mbolea.


Mbunge huyo ameipongeza serikali kuongeza bajeti ya Kilimo kutoka Bilioni 294 mpaka Bilioni 954 na kudai kuwa kuongezwa kwa bajeti hiyo ni uthubutu mkubwa na kutaka kuhakikisha wanapokea fedha hizo ili yale mafanikio ambayo wanategemea wakulima yafikiwe.


Alisema kuwa, kutoa mbolea kwa wakulima pekee bila kuwapatia mbegu bora na viwatilifu uzalishaji unaweza usifikie kiwango ambacho serikali inatarajia.


Kuhusu kilimo cha  umwagiliaji amesema kuwa, mabadiliko ya tabia ya nchi yamesababisha shida kubwa na kupelekea upungufu wa chakula karibu dunia nzima hivi sasa.


Amesema kuwa, yapo maeneo mengi yenye maji ya kutoka katika vyanzo mbali mbali  na kuipongeza Wizara ya Kilimo kwa kuwa na miradi 36 ya skimu za umwagiliaji.


Mbunge huyo ameowaomba katika mpango huu kuhakikisha wanajenga miradi mipya ya umwagiliaji kwenye maeneo ambayo yana maji ya kutosha ili kuweza kunufaika na Kilimo cha umwagiliaji pamoja na kuongeza fedha katika umwagiliaji.


Kuhusu kilimo cha bustani amesema kuwa, hivi karibuni kumezinduliwa mpango wa taifa wa kilimo cha bustani ambapo kilimo hicho cha mboga mboga ndio kitu ambacho kinaweza kulikwamua taifa kwa sababu mbogamboga zinasoko kila mahali.


Prof. Ndakidemi ameiomba serikali kwenye huo mpango kuhakikisha wanafuatilia ili mpango huo unatekelezwa pamoja na kuhakikisha wananchi wanazalisha mbogamboga na matunda.


Katika hatua nyingine Prof Ndakidemi amesema kuwa wametembelea vituo vya utafiti wa kilimo TARI lakini miundombinu ya vituo hivyo ipo hoi na taabani.


Amesema kuwa, Tanzania vipo vituo vya utafiti 17 ambavyo miundombinu ya ofisi haijakaa vizuri huku Maabara ni kama hazipo kabisa pamoja na nyumba za watumishi kutokuwa vizuri.


Amesema kuwa, bila utafiti hakuna mahali tutakwenda na kudai kuwa nchi nyingi zimefanikiwa duniani kutokana na utafiti hivyo kuwaongezea fedha za kutosha kufanya utafiti kwenye mbegu na kubuni mbinu bora za kuongeza tija kwenye kilimo taifa litanufaika.

Share To:

Post A Comment: