Na John Walter-Manyara

Mkuu wa Mkoa wa Manyara (RC), Makongoro Nyerere amewatuhumu Mbunge wa Jimbo la Babati mjini Pauline Gekul na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Babati Abdulrahaman Kololi kwa kuchochea migogoro ya ardhi kwenye shamba la mwekezaji Dudumera lililopo Kata ya Maisaka.

Makongoro akizungumza  kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa huo (RCC) kilichofanyika mjini hapa, amesema Viongozi hao wawili  wanatuhumiwa na Makongoro kuwachochea wananchi ili wavamie shamba la hilo ambalo bado  ni mali ya mwekezaji na kusababisha vurugu.

Amemwagiza kamanda wa polisi mkoa wa Manyara kuwakamata watu wanaovamia eneo hilo.

 

Makongoroi amesema hawezi kuvumilia viongozi wanaosababisha migogoro “hata kama ni mwenyekiti wa halamshauri kamata peleka magereza,tutampata mwingine” alisisitiza Makongoro.

 

"RPC mkawakamate hao vijana kwani mbunge anahusika na diwani anahusika kuchochea mgogoro ni bora akose hiyo nafasi ili uchaguzi ufanyike na tupate Mwenyekiti mpya wa halmashauri ya mji," amesema Makongoro.

 

Hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan  alifanya ziara ya siku mbili kutembelea mji wa Babati ambapo katika hotuba yake akizungumza na wananchi kwenye mkutano uliofanyika uwanja wa Kwaraa, alitoa onyo kwa viongozi kutochochea migogoro ya ardhi.

 

Hata hivyo, Kololi amesema yeye hawezi kuzungumzia chochote juu ya shutuma hizo huku Gekul akisema anashangazwa na shutuma hizo kwani yeye amekuwa mpatanishi wa tatizo hilo na siyo kuchochea migogoro ya ardhi.

 

"Juzi kulitaka kuzuka vurugu pale juu ya mgogoro huo, nilifika na polisi tukawapooza wananchi, leo inakuwaje nasingiziwa kuanziaha mgogoro huo," amehoji Gekul.

 

Amesema wananchi hao hawajavamia eneo hilo kwani walikuwepo zaidi ya miaka 70 iliyopita hivyo hawapaswi kuondolewa hivi sasa labda wapewe sehemu nyingine ya kufidiwa.

 

Share To:

Post A Comment: