Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo barani Afrika (WiLDAF) limeandaa msafara wa siku 16 unaozunguka katika mikoa saba nchini Tanzania (Pwani, Morogoro, Singida, Shinyanga, Geita, Mara na Arusha) kwa ajili ya kupaza sauti ya kupinga ukatili wa kijinsia. 

Msafara huo ambao unahusisha wadau mbalimbali wa maendeleo na viongozi wa Serikali umezinduliwa na Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Doroth Gwajima tarehe 25.11.2022 katika  viwanja vya Leaders Club vilivyoko Kinondoni, Jijini Dar es Salaam na utahitimishwa tarehe 10.12.2022 Jijini Arusha. 

Msafara huo unaongozwa na kauli mbiu ya mwaka 2022 ya kupambana na ukatili wa kijinsia inayosema; “Kila Uhai una thamani, tokomeza mauaji na  ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto”. 

Mapambano haya sio mapya, kinachofanyika Tanzania leo ni muendelezo wa kampeni ya kimataifa  iliyoanzishwa na kituo cha kimataifa cha wanawake katika uongozi (Women’s Global Leadership)  mwaka 1991 kwa lengo la kukemea vitendo vya ukatili wa kijinisia duniani kote ili kuifanya dunia iwe sehemu salama kwa binadamu wote. 

Mbali na kujenga nguvu ya pamoja na kupaza sauti kukemea matendo ya ukatili wa kijinsia nchini Tanzania msafara huu pia unalenga yafuatayo: 

Kutoa elimu kwa wananchi  wa rika mbalimbali wakiwemo  wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili kujenga uelewa kuhusu ukatili wa jijinsia.

Kutambua vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyojitokeza katika mkoa na maeneo husika. 

Kutambua mbinu wanazozitumia kukabiliana na vitendo hivyo katika maeneo yao.

Kutambua changamoto wanazokubana nazo wakati wa mapambano ya ukatili wa kijinsia.

Kutambua misaada wanayopatiwa wahanga wa ukatili wa kijinsia katika maeneo yao.

Kujadiliana na kutoa mapendekezo ya mbinu bora zinazoweza kutumika kutokomeza ukatili wa kijinsia.

Tayari msafara umeshatembelea mikoa miwili, ambayo ni; Pwani na Morogoro na kupeleka elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia. 

Katika Mkoa wa Pwani Msafara ulitembelea wananchi wanaozunguka soko la Loliondo, Kibaha na Shule ya Msingi Tumbi. Mkoani Morogoro Msafara ulifika na kutoa elimu kwa wananchi wanaozunguka soko la Chief Kingalu na Shule ya Sekondari Mwembe Songo. Kwa ujumla,  maeneo yote yaliyotembelewa, wananchi na wanafunzi walisema kuwa tatizo la ukatili wa kijinsia bado lipo kwa kiwango kikubwa. Kwa mfano: vitendo vya ubakaji wa watoto, vipigo kwa wanawake na watoto, ulawiti kwa watoto wa kike na kiume, matusi  vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku.

 Vitendo hivyi vimekuwa vikifanyika majumbani na shuleni na vinafanywa na marafiki au ndugu wa karibu na hivyo watuhumiwa na wahanga wamekuwa wakilindana na kukwepa mkono wa sharia kutokana na ukaribu walio nao. 

Hii tabia ya kulindana imeleta changamoto katika harakati za mapambano ya vitendo hivyi na hivyo kufanya tatizo liendelee kuwa sugu.  Kwa maoni yao wananchi na wanafunzi wanapongeza jitihada za Wizara na Shirika la WiLDAF pamoja na wadau wengine wa maendeleo kwa jitihada hizi za kupinga ukatili wa kijinsia. 

Wanasema, Msafara huu wa kupinga ukatili wa kijinsia umewafikia wakati muafaka ambapo wanahitaji jamii ilimishwe ijue madhara ya vitendo hivyo na mbinu za kukabiliana navyo.Share To:

Post A Comment: