Na John Walter-Manyara 

 Imeripotiwa watu sita wamefariki dunia na watano kujeruhiwa katika ajali iliyotokea kwenye kijiji cha Kimana kata ya Partimbo tarafa ya Kibaya wilayani Kiteto mkoani Manyara baada ya gari aina ya Land cruiser Prado Tx yenye namba za usajili T 323 DWP kugongana uso kwa uso na gari aina ya Land cruiser inayotumika kubebea wagonjwa mali ya halmashauri ya wilaya ya Kiteto. 

 Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo Kamishna msaidizi wa polisi mkoa wa Manyara George Katabazi amesema waliopoteza maisha wote walikuwa kwenye gari ya kubebea wagonjwa huku watano kati yao ni madaktari na mmoja ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi Asamatwa. 

 Kamanda Katabazi ameeleza chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa gari aina ya Land cruiser Prado Tx kutaka kulipita basi lililokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari hali iliyopelekea kugongana uso kwa uso. 

 Aidha kamanda Katabazi ametoa wito kwa madereva wa vyombo vya moto na watumiaji wengine wa barabara kuchukua tahadhari za usalama barabarani na kuendesha vyombo vya moto kwa kuzingatia sheria na taratibu za usalama barabarani. 

 Waliofariki Joseph Buzuku (36), Edward Makundi (47), Kidd Said (36), Selina Nyimbo (31), Catherine Tadei (31) wote watumishi wa kituo cha Afya Sunya wilayani Kiteto pamoja na Agapti Kimaro (32) mwalimu mkuu shule ya Msingi Asamatwa. 

 Waliojeruhiwa Ibrahim Selemani (71) mkazi wa Makuyuni Korogwe Tanga, ameumia kifuani na kulazwa katika Hospitali ya wilaya Kiteto, Method Makiri (55) ambaye ni dereva mkazi wa Sinza Dar es Salaam amevunjika mguu wa kulia na kukimbizwa Dodoma kwa matibabu zaidi, Mbaraka Shaban (44) mkazi wa Kimara Dar es Salaam, amepata majeraha kichwani na kulazwa hospitali ya wilaya Kiteto, Juma Mbaruku (45) dereva mkazi wa Sunya Kiteto amevunjika miguu yote na amepelekwa Dodoma, Nickson Muhongw’a (36) Daktari mkazi wa Sunya Kiteto ameumia Kifua,kichwani na mbavu, amepelekwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma.
Share To:

Post A Comment: