Jumla ya watu 1233 wamefanyiwa upimaji na matibabu ya moyo katika kambi maalum ya matibabu iliyofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC).


Kambi hiyo ya matibabu ya moyo iliyofanyika kwa siku tano ilianza tarehe 26 hadi 30/09/2022 ambapo watu wazima pamoja na watoto walipata matibabu. Kambi hii ilikuwa ni maalum kwa ajili ya kuadhimisha siku ya moyo duniani iliyofanyika tarehe 29/09/2022.

Kwa upande wa watu wazima waliofanyiwa upimaji wengi wao walikutwa na matatizo ya shinikizo la juu la damu, kutanuka kwa moyo, kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo na shida za valvu za moyo.

Watoto 70 walifanyiwa uchunguzi ambapo wengine walikutwa na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa katika mpangilio wake pamoja na valvu za moyo kuwa na shida.

Wagonjwa wengine kwa mara ya kwanza wamegundulika kuwa na matatizo ya moyo ikiwa ni pamoja na kutanuka na kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo ambapo asilimia 5 tumewapa rufaa ya kuja kufanyiwa vipimo zaidi na kutibiwa katika Taasisi yetu.

Kwa upande wa watoto wenye matatizo tumewaelekeza kuja JKCI ili waweze kufanyiwa upasuaji katika kambi maalum za upasuaji wa moyo kwa watoto zitakazoanza tarehe 10/10/2022 na wengine watahudhuria kliniki zetu kwa ajili ya matibabu na kuwafuatilia kwa ukaribu zaidi.

Katika kambi hii wananchi walipimwa vipimo mbalimbali vya moyo ikiwa ni pamoja na urefu, uzito, kiwango cha sukari mwilini, kuangalia uwiano baina ya urefu na uzito, kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography), mfumo wa umeme wa moyo (Electrocardiography) pamoja na vipimo vya damu (utendaji kazi wa figo, ini na kiwango cha mafuta kwenye damu).

Tulikuwa na wataalamu wa lishe ambao walitoa elimu ya lishe bora ambayo iliwapa wananchi kuwa na uelewa wa kufuata mtindo bora wa maisha ambao utawasaidia kuepukana na magonjwa ya moyo ambayo ni moja ya magonjwa yasiyoambukiza na mtu anaweza kuyaepuka kwa kufuata ushauri wa kitaalamu.

Wananchi waliopata huduma za matibabu walitoka katika mikoa ya Arusha, Shinyanga, Singida, Mara, Kagera, Morogoro, Tanga, Manyara, Kilimanjaro na Iringa. Tumeona kuna uhitaji mkubwa wa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo hiyo basi Taasisi yetu itaendelea kuwasogezea wananchi huduma hizi kwa kuwafuata mahali walipo.

Pia tutawajengea uwezo wataalamu wa afya wa jinsi ya kutambua na kutibu magonjwa ya moyo kwani Serikali imenunua mashine za kisasa za kuchunguza moyo na kuzisambaza katika Hospitali mbalimbali hapa nchini.

Tunawaomba wananchi muepuke tabia hatarishi zinazoweza kuharibu mioyo yenu hii ikiwa ni pamoja na uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe uliokithiri. Zingatieni mtindo bora wa maisha kwa kufanya mazoezi na kula vyakula bora.

“Tunajali Afya ya Moyo Wako”.
Share To:

Post A Comment: