Na Joel Maduka Geita. 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amelitaka Shirika la  Madini la Taifa  (STAMICO) kuutangaza mkaa mbadala wa Rafiki Briquettes  ili kuhamasisha matumizi yake kwa wakazi wa Geita 

Hayo ameyasema alipokuwa ametembelea banda la STAMICO na kujionea  jinsi ilivyojipanga kutoa elimu wakati wa maonesho ya Tano ya Madini  yanayoendelea mkoani Geita. 

Amesema ni muhimu  kuutangaza mkaa huo ili watu waufahamu na kuanza kuutumia ili kuweza kuokoa mazingira kwa kupunguza matumizi ya mkaa utokanao na miti.

Katika hatua nyingine Mbibo amefungua Semina ya Wachimbaji na kusema, lengo la semina hiyo ni kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata elimu na ujuzi wa namna bora ya utafiti, uchukuaji wa sampuli, uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

Ametoa wito kwa wachimbaji wadogo kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika semina hiyo kwa lengo la kujipatia elimu na ujuzi wa namna bora ya uendeshaji wa shughuli zao.

Aidha, Mbibo ameiagiza STAMICO pamoja na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kuendelea kutoa elimu ya namna ya kufanya tafiti na uchukuaji wa sampuli.

Sambamba na hayo , Mbibo ameupongeza mkoa na wilaya ya Geita kwa kuendesha zoezi la uandaaji wa Maonesho ya 5 ya Teknolojia ya Madini 2022.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Geita Shimo William amempongeza Mbibo kwa kukubali kufungua semina hiyo na kuahidi kuendelea kuwalea na kuwasimamia vyema wachimbaji wadogo wa mkoa huo.




Share To:

JUSLINE

Post A Comment: