Na Gift Mongi Moshi

Wananchi wa kata ya Kibosho Kirima hususan katika kijiji cha Boro katika halmshauri ya Moshi mkoani Kilimanjaro wapo mbioni kupata umeme wa uhakika kutokana na zoezi la uunganishaji   wa nishati hiyo unaoendelea hivi sasa.

Kukamilika kwa zoezi hilo ni dhahiri pasipo na mashaka kuwa fursa zaidi za kiuchumi zitaenda kufunguka katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na kufungua milango ya ajira pamoja na kujiajiri kwa vijana.

Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo unaoendelea kutekelezwa mbunge wa jimbo la Moshi vijijini Profesa Patrick Ndakidemi  amesema kuwa eneo hilo la kata ya Kibosho Kirima kulikuwa na shida ya kukatika umeme kwa kipindi kirefu kutokana na umeme kuwa kidogo na wateja kuwa wengi.

Prof Ndakidemi ambaye pia ameongozana na  meneja wa shirika la umeme (TANESCO) mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Abdulrahman  Nyenye ni kuwa tayari mradi huo umeshakamilika kwa zaidi ya asilimia 80. 

Aidha Prof Ndakidemi ameishukuru serikali kwa jinsi ambavyo serikali imetekeleza ahadi ya kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika jimbo la Moshi vijijini.

Amesema kutokana na kasi hiyo inayoendelea wakazi wa jimbo hilo  wana mategemeo makubwa ya  ongezeko la umeme pindi mradi huo utakapokamilika ambapo wananchi wanategemea kujiajiri kwa kuanzisha miradi  mbalimbali ya kijamii katika kijiji cha Boro.

Kwa upande wake Mhandisi Nyenye amemhakikishia mbunge huyo na wananchi kwa ujumla kuwa zoezi hilo litaenda kukamilika kwa wakati na kuwa adha ya upatikanaji wa nishati hiyo kwenye kijiji hicho kutaenda kubaki historia.

Calvin Mushi mkazi wa kijiji hicho amesema kupatikana kwa nishati ya umeme katika eneo hilo kutawezesha kukuza biashara mbalimbali hususan zile zenye uhitaji wa nishati hiyo.

Amesema kwa mara kadhaa vijana wameshindwa kujikwamua kiuchumi kwani biashara nyingi zikiwemo za saloon,ufundi vyuma,mabucha ya kuuza vitoweo vyote vikihitaji umeme wa uhakika na kuwa wengi walishindwa kuzifanya kwa kuhofia kupata hasara.

Share To:

Post A Comment: