Na DENIS CHAMBI, TANGA, 


BWAWA la maji Horohoro Boda mpakani mwa Tanzania na Kenya linalotegemewa na wananchi zaidi 7000 limeanza kukauka kufuatia ukame na kusababisha taharuki kwa wananchi wa vijiji zaidi ya sita wanaotegemea bwawa hilo.

Bwawa hilo wanalitegemea kwa maji ya matumizi ya nyumbani na mifugo.

Hali ya ukame imejatwa kama sababu muhimu inayosababisha  bwaha hili kukauka na kusababisha tabu ya maji kwa matumizi ya binadamu na mifugo.

Vijiji kadhaa vinavyotegemea bwawa hilo hofu imeanza kutanda  kwamba ni wapi watapata huduma hiyo.

Wakizungumza na kituo hiki kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wa enei hilo akiwemo Halid Hakim ambaye ni mkazi wa Horohoro Boda, amesema tegemeo kubwa la maji ni bwawa hilo ambalo kipindi cha mvua linajaa na kusaidia wananchi wengi wakiwemo wa nchi jirani ya Kenya wa vijiji vya Lungalunga na Jua Kali.

"Wenyewe mnashuhudia maji yamebaki machache unaweza kuyaona ni machafu lakini ndiyo tunayokunywa na kuyafanyia shughuli zote za kibinadamu," amesema Hakim

Aidha amesema suala la maji katika mji wa Horohoro linalohitaji serikali ilitatue kwa haraka ili wananchi waweze kupata ustawi katika maisha yao ya kila siku.

Mkazi mwingine wa Horohoro Kijijini, Rajab Jumaa amesema kuwa wanachangamoto kubwa ya maji kwa matumizi yao na wanaiomba serikali iwasaidie ili waweze kutegemea kutumia maji yanayopatikana wakati wa majira ya mvua tu.

"Tunaomba Serikali sasa ione tatizo hili ni kubwa na lifikie kikomo, sisi hapa Horohoro tunakunywa maji kutegemea misimu ya mvua tu, hatuwezi kuishi hivi kwa kubahatisha kama wataalamu wanavyosema maji ni uhai, watusaidie tuondokane na hii hali," amesema na kuongeza, "Ukiyatazama haya maji huwezi kuamini kwamba ndiyo tunayokunywa,".

Amesema ni wakati wa serikali kuinua macho kuutazama mji wa Horohoro ambao kiukweli kutokana na changamoto ya maji umekuwa ukikosa kukua kwa wageni kushindwa kujenga nyumba za kuishi pamoja na nyumba za biashara licha ya kuwepo ofisi za serikali za idara mbalimbali ikiwemo mamlaka ya mapato TRA inayokusanya kodi.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Duga Miliya Merimeri, ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia kuwaptia fedha hizo ili kumaliza changamoto ya bwawa hilo ambalo litakapokamilika litamaliza matatizo ya maji katika kata hiyo yenye vijiji vinne.

"Tunamshukuru Rais wetu mama Samia suluhu Hassan kwa kutupatia fedha za kuendeleza mradi wa bwawa letu ambalo ukarabati wake utakapokamilika utasaidia wananchi wengi wakiwemo wa nchi jirani," amesema.

"Tatizo la maji ni kubwa sana hapa Horohoro kwa wakazi wangu zaidi ya Vijiji sita pamoja na vile vya nchi jirani ya Kenya, tunaishi kutegemea bwana hili" amesema.

Amesema kwa ujumla idadi halisi ya wakazi katika eneo hilo ni watu 3,000 lakini ukichanganya na Vijiji vya nchi jirani ya Kenya wanafika watu 7,000 hadi 8,000 ambao ndiyo wanapata maji katika bwawa hilo.

Bodi ya bonde la Pangani inatembelea eneo hili  na kutoa matumaini  kwa wananchi ambapo Mwenyekiti wa Bodi ya maji ya bonde la Pangani Mhandisi Ruth Koya ameishukuru serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa miradi ya maji ili kutatua changamoto ya maji kwa wananchi katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Sambamba na hayo amesema bonde la Pangani lenye jukumu la kusimamia vyanzo vya maji, litahakikisha inaisimamia serikali katika utekelezaji wa miradi ya maji na amewaomba wananchi wawe na subira wakati serikali inafanya mchakato wa kumaliza changamoto za maji katika maeneo yao.

Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani, Segule Segule amesema mpango wa bonde ni ukarabati kuliwezeasha bwawa hilo kutunza maji kwa kipindi kirefu hadi kipindi cha kiangazi kuanzia mwezi januari mwakani. 

Mkurugenzi Segule amesema serikali ya Rais Samia tayari imetoa kiasi cha shilingi bilioni 1.89 kwa ajili ya kulikarabati bwawa hilo liweze kuwa na maji yatakayosaidia wananchi majira yote ya masika na kiangazi 

Hata hivyo amesema kazi ya kukarabati bwawa hilo imeanza mapema Januari mwaka huu baada ya kuunda kamati ya watu wa wizara ya maji, Tanga Uwasa na Bonde hilo walifika kufanya usanifu wa ujenzi wa bwawa hilo na kwamba sasa wataanza ujenzi wake.

Vijiji vinavyo tegemea bwawa hilo ni pamoja na kijiji cha Mailnane,Jua kali ,Lungalunga  upande wa Kenya ,Ngazini   na Horohoro.

Share To:

Post A Comment: