DENIS CHAMBI, TANGA.

Serikali imetoa fedha zaidi ya bilioni 200 kwa ufadhili wa World Bank katika mwaka huu wa fedha kwa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira jijini Tanga (Tanga Uwasa) kwajili ya kukarabati mfumo wa maji taka katika jiji la Tanga na pia kuendeleza maeneo ambayo mtandao huo haujafika.


Mradi huo utahusisha ujenzi wa mabwawa ya kisasa ya kutibu maji taka na kutoa vifaa vya utendaji kazi kama mashine za kusafisha mtandao wa maji taka mashine za kuzibulia mikwamo. 


Hayo yamebainishwa na Mhandisi Abdul Ramadhani ambaye ni msimamizi wa mfumo wa maji taka Tanga Uwasa wakati wa wakiadhimisha wiki ya huduma kwa Wateja iliyoambatana na mkutano wa hadhara na wananchi wa kata Ngamiani, mtaa wa Lumumba lengo kuu ikiwa ni kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya mtandao wa Majitaka sambamba na huduma ya majisafi.


Mhandisi Ramadhani amesema kuwa  kwa sasa mradi hui upo kwenye hatua za awali za usanifu ambapo wamepata mkandarasi mshauri kutoka serikali ya India ambaye anafanya usanifu hivi sasa huku matarajio yakiwa ifikapo mwanzoni mwa mwaka ujao atakuwa amemaliza usanifu na hatimaye taratibu za kufanya zabuni za kumpata mkandarasi mjenzi zitaanza mara moja. 


"Hii ni bahati ya kipekee kwa wakazi wote wa jiji la Tanga kwa maana wanakwenda kupokea mradi mkubwa ambao unakwenda kubadilisha hali ya kimazingira katika jiji la Tanga hususani katika uondoshaji wa maji taka, "alibainisha Mhandisi Ramadhani. 


Aidha amesema mradi huo utahudumia wakazi wote wa jiji la Tanga ambapo utahudumia zaidi ya asilimia 80 na maeneo ambayo hayatafikiwa na mtandao kutakuwepo na mradi mwingine katika sehemu ya mradi huo huo utakaohudumia maeneo ya kando kando ya nje ya jiji la Tanga. 


Devotha Mayala ni Mkuu wa kitengo cha  mawasiliano na uhusiano kutoka Tanga Uwasa amesema wamekutana na wakazi wa maeneo hayo ya Ngamiani kati kwajili ya kutoa elimu lengo kuu likiwa ni kutoa elimu juu ya huduma ya maji taka huku wakigusia kipengele cha bili za maji ambapo wamepata elimu ya namna ya kusoma mita za maji lakini pia wamepata kufahamu utaratibu mzima ulivyo wa bili zinavyoandaliwa mpaka kuwafikia wateja. 


"Tumefarijijka sana kukutana na wananchi hawa wa Ngamiani kati lakini pia tumefurahi kupokea maoni kutoka kwao kwasababu ni lengo jingine la Taasisi tunapoandaa shughuli kama hizi kwamba tupokee maoni taarifa na hata kero kutoka kwa wananchi kuhusiana na huduma tunazozitoa Tanga Uwasa, "alisisitiza Mayala. 


Kwa upande wake Meneja wa huduma kwa wateja Tanga Uwasa Rogers Machaku amesema kuwa wamekuwa wakitoa elimu mbalimbali ya kuelezea shughuli zao na kuelimisha wananchi juu ya kutumia maji sahihi pamoja na kutumia mfumo wa majo taka sahihi. 


"Tumeona tushiriki na Taasisi zingine katika wiki hii ya huduma kwa wateja tumekuwa na ratiba ya kutembelea baadhi ya maeneo kukutana na watu moja kwa moja na kwenye wiki hii tumekuwa na vituo viwili ikiwemo Mwakidila sokoni tumekuwa na wananchi wa pale na tumeweza kusikiliza kero zao na ushauri ili tuweze kuboresha huduma zetu, "alisema Machaku. 


Baadhi ya wananchi wa eneo hilo la Ngamiani kati akiwemo Mohamed Sadick na Subira Ally wameipongeza Tanga Uwasa kwa kuwa karibu na wateja wao jambo ambalo linazidi kuwapa imani kubwa na mamlaka hiyo. 


Katika mkutano huo wananchi pamoja na kupatiwa elimu juu ya huduma za Tanga Uwasa pia walipata fursa ya kutoa maoni, kuuliza maswali na kuwasilisha kero, taarifa na malalamiko juu ya huduma zinazotolewa na Tanga Uwasa. 

Share To:

Post A Comment: