Waziri Jenister Mhagama katika moja ya hafla ya kuhamasisha matumizi ya Lishe bora kwa watoto

Lishe ina uhusiano na afya ya akili_ hivyo mtoto anahitaji lishe kamili ili kuwa na afya njema pamoja na akili timamu.

Watoto wadogo wanapata lishe bora kwa kula milo iliyo kwenye makundi yote matano ya vyakula kama inavyoonekana katika picha hii. 

Na Abby Nkungu, Singida 

ASILIMIA 97 ya watoto wenye umri chini ya miaka miwili mkoani Singida hawapati mlo kamili unaokubalika na waatalamu wa lishe bora, hali inayochangia kupata changamoto mbalimbali za kiafya; ikiwemo udumavu, ukondefu na uzito mdogo.

Taarifa ya Utafiti wa Kitaifa wa Lishe (TNNS) uliofanyika mwaka  2018, inaonesha kuwa ni asilimia tatu tu (3%) ya watoto wenye umri wa chini ya miaka miwili mkoani Singida ndio wanaopata mlo unaokubalika kilishe.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Victorina Ludovick ilieleza kuwa lishe duni ni moja  ya sababu zinazochangia kuendelea kuwepo kwa tatizo la udumavu mkoani humo kwa asilimia 29.8, ukondefu asilimia 4.7 na uzito pungufu asilimia  14 kwa watoto walio chini ya miaka mitano.

Hata hivyo, alisema kuwa pamoja na hali kuwa bado sio ya kuridhisha, matatizo hayo yamepungua ikilinganishwa na miaka minne kabla ya kutafiti huo (yaani 2014) ambapo  udumavu ulikuwa asilimia 34, ukondefu asilimia 5 na  uzito mdogo asilimia 15.

“Maendeleo sio mabaya. Hii Programu Jumuishi ya Taifa ya miaka mitano juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto itasaidia kuleta matokeo chanya zaidi katika suala la lishe kwani inahusisha masuala mtambuka” alisema na kuongeza kuwa ni suala la muda tu kumaliza changamoto hiyo.

Alieleza kuwa chini ya Programu hiyo, wadau wamekuwa wakiunganisha nguvu kwa ajili ya kushughulikia masuala ya kuimarisha ulinzi kwa watoto wenye umri chini ya miaka minane, afya, lishe, elimu na masuala mengine mtambuka kwa kundi hilo muhimu katika jamii.

Alisema kuwa, pamoja na wadau wengine kutimiza vyema wajibu wao kupitia Programu Jumuishi ya Taifa, Serikali nayo imeongeza bajeti ya lishe kwa mtoto kwa kila  halmashauri kutoka 1,000/- kwa mwaka wa fedha 2020/21 hadi 1,239/- kwa mwaka 2021/2022.

Wataalamu wa afya ya Mama na Mtoto wanasema kuwa pamoja na udumavu, ukondefu na uzito pungufu, suala la lishe duni ni miongoni mwa sababu za homa za mara kwa mara kwa mtoto.

“Lishe duni ni chanzo mojawapo cha magonjwa na vifo kwa watoto wadogo; hasa walio chini ya miaka mitano. Pia hudumaza ukuaji wa kimwili na kiakili" alisema Dk Suleiman Muttani, Daktari Bingwa Mshauri wa magonjwa ya wanawake na watoto hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Singida.

"Kama hiyo haitoshi, lishe duni pia hupunguza uwezo wa mtoto kufanya vizuri awapo shuleni na ufanisi wa kazi katika maisha yake ya utu uzima hapo baadae" aliongeza Dk Muttani.

Wazazi, walezi na wataalamu kutoka Mashirika, Asasi na Taasisi zinazoshughulikia ustawi wa mtoto, wanasema njia pekee ni kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa lishe bora kwa mtoto  ndani ya siku 1,000 za awali ili kujenga afya bora.

“Unaweza kushangaa tatizo kubwa la lishe duni kwa watoto lipo vijijini kuliko mjini wakati huko ndiko vyakula vingi vya asili na vyenye virutubisho vinapatikana. Kwa hiyo, shida ni elimu kwa jamii” Mama Amina Ali wa Kibaoni Singida mjini alisema.

Ofisa Maendeleo ya Jamii mstaafu na Mtafiti wa masuala ya mila na desturi za Wanyaturu, Patrick Mdachi alisema imani potofu miongoni mwa jamii; hasa vijijini juu ya ulaji wa baadhi ya vyakula muhimu vinavyoshauriwa na wataalamu wa afya ili kujenga mwili wa mjamzito na mtoto, ni kikwazo kingine.

“Huwezi kuamini ila jaribu kutoka nje kidogo ya mji.  Kuna wajawazito na watoto hawali mayai, maini,  firigisi na vyakula vingine vingi muhimu eti kwa kukatazwa na Wazee wa kiume. Hii inaturudisha nyuma sana” alieleza Mdachi na kutaka wadau kushirikiana na Viongozi wa dini, Wazee wenye uelewa na wataalamu wa afya kukemea mila hizo potofu. 

Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: