Mmoja wa watoto akionesha majeraha yaliyotokana na kufanyiwa ukatili na ndugu zake.
Ukatili kama huu kwa watoto haufai na kwa mujibu wa Wataalam waafya una athari kwa makuzi ya mtoto
Wanafunzi wa shule moja hapa nchini wakiwa wameshika mabango yanayokemea ukatili kwa watoto.
.

Na Abby Nkungu, Singida


UKATILI wa kijinsia na unyanyasaji kwa watoto wenye umri chini ya miaka minane  umepungua kwa zaidi ya asilimia 47 katika halmashauri za Wilaya ya Singida, Ikungi na Manyoni mkoani Singida kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.

Taarifa rasmi iliyotolewa na Mkuu wa dawati la jinsia la Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, Mkaguzi wa Polisi Amina  Bendera inaonesha kuwa,  vitendo hivyo vimepungua kutoka makosa 154  kuanzia Januari hadi Juni mwaka jana 2021 na kufikia makosa 81 kwa kipindi kama hicho mwaka huu.

Katika taarifa hiyo, Mkaguzi wa Polisi Amina amefafanua kuwa halmashauri ya Wilaya ya  Singida kuanzia Januari hadi Juni mwaka jana iliripoti matukio 100 ya ukatili wa kijinsia  na unyanyasaji kwa watoto wa chini ya miaka minane lakini mwaka huu kwa kipindi hicho yameripotiwa makosa 38 tu.

Alieleza kuwa katika wilaya ya Ikungi  makosa hayo yamepungua kutoka  30 mwaka jana hadi 23 mwaka huu wakati  Manyoni  takwimu zinaonesha kupungua kwa matukio hayo ya  ukatili kutoka 24 hadi 20 Juni mwaka huu.

Mkuu huyo wa dawati la jinsia la Polisi mkoa wa Singida, aliyataja baadhi ya makosa hayo kuwa ni pamoja na ubakaji, kujaribu kubaka, kulawiti, kunajisi, ukeketaji, vipigo na kujeruhi watoto.

Alisema kuwa pamoja na usimamizi na utekelezaji wa sheria unaofanywa na vyombo mbalimbali, juhudi kubwa za Serikali na wadau wake katika kutoa elimu kwa jamii juu ya kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto ni miongoni mwa sababu za kuanza  kupungua kwa vitendo hivyo.

“Kuna hii Programu Jumuishi ya Taifa juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto iliyoanza kutekelezwa Januari mwaka jana na inaendelea hadi mwaka 2026, imesaidia sana kufikia mafaniko hayo maana kila mdau wa mtoto anatekeleza vyema wajibu wake katika eneo la malezi, ulinzi, afya, lishe, elimu na mengine mengi; hivyo kufanya kazi yetu kuwa rahisi” alisema Inspekta Amina

Hata hivyo, wadau wanasema kuwa pamoja na taarifa ya polisi kuonesha mafaniko hayo ya kuanza kupungua kwa matukio ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto,  bado  kuna haja ya kuongeza nguvu zaidi ya elimu katika jamii ili kupinga na kutokomeza kabisa uhalifu huo.

“Sisi  ndio  tupo katika jamii, tunaona na kusikia mengi, bado vitendo hivyo vipo isipokuwa sio vyote vinavyoripotiwa kwenye ofisi za Serikali, polisi au vyombo vingine vya sheria. Wengine wanamaliza nyumbani  kesi hizo kwani hufanywa na ndugu wa karibu” alisema Magdalena Soteri mkazi wa  Kindai mjini Singida na kuungwa mkono na Ramadhani Hamisi wa eneo la Unyankhae.

“Ni elimu tu hakuna njia nyingine kama kila mtu kuanzia mzazi, mlezi na jamii nzima atakuwa mlinzi wa mtoto na kutooneana huruma na kumaliza kindugu kwa mtuhumiwa anayetenda makosa hayo ni dhahiri kuwa vitendo hivyo vitabaki kuwa historia katika jamii yetu” alisisitiza Ramadhani.

Watalamu wa afya wanasema kuwa zipo athari nyingi ambazo huwakumba watoto waliofanyiwa ukatili wa kijinsia na unyanyasaji zikiwemo za kisaikolojia, kimwili, kiafya, na kiakili.

Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto inasema utafiti mdogo uliofanywa na Benki ya Dunia kwenye jamii kuhusiana na ukatili, unyanyasi na utelekezaji watoto wadogo unaofanywa na wazazi mkoani Katavi ulionesha asilimia 18 ya wazazi wenye watoto chini ya miaka mitatu kuwapiga vibao watoto wao.

Nazo tafiti za awali za mradi wa malezi uliofanywa na Shirika la EGPAF wilayani Nzega, Igunga na Tabora Manispaa uliripoti kuwa asilimia 53 ya wazazi wa watoto wenye umri wa miaka 0 - 2 wanaamini kuwa watoto lazima waadabishwe kwa kuchapwa.

Hata hivyo, hakuna takwimu zinazoonesha picha halisi ya ukatili, unyanyasaji na utelekezaji watoto Kitaifa. 

 

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: