Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde (Mb) amewataka watu wenye ulemavu kutumia maarifa watakayopewa kwenye mafunzo ya kilimo ili kujikimu kiuchumi na kujiondoa kwenye umaskini unaopelekea unyanyapaa.


Mhe. Mavunde ameyasema hayo jana tarehe 28 Septemba, 2022 alipokuwa akifungua Kongamano la Kilimo kwa Watu Wenye Ulemavu katika ukumbi wa Royal Village, Jijini Dodoma.

"Azma ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni kukuza sekta ya kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030. Katika kufikia hilo, niwahakikishie kuwa makundi maalum yote yanashirikishwa wakiwemo watu wenye ulemavu.

Mhe. Rais ameongeza bajeti ya Kilimo kutoka bilioni 294 mwaka 2021/2022 hadi bilioni 954 mwaka 2022/2023, hii inaonesha kuwa Serikali imeweka mkazo mkubwa kuwezesha wananchi wengi ambao ni wakulima kupata faida kupitia kilimo. Mafunzo ya leo, yatawaongezea maarifa watu wenye ulemavu ambayo yatakuwa kama silaha ili kwenda kuleta matokeo chanya kwenye sekta ya kilimo na kujikimu.

Hakuna kinachoshindikana chini ya jua, natamani kuwaona siku moja mkiwa wakulima wakubwa, mkiwa mnasambaza mbolea na madawa mbalimbali. Nataka niwatie shime kuwa kilimo mkikifanya kibiashara kinalipa sana. Kampuni ya SBL nawasihi sana sana mfanye zaidi ya mafunzo, muwakuze washiriki hawa wa mafunzo, muwape kipaumbele zaidi kundi hili la watu wenye ulemavu ili likawe mfano wa kuigwa na wengine.

Vilevile kwa upande wa Serikali, tutahakikisha kuwa tunatenga maeneo kwa ajili ya watu wenye ulemavu na kuwaunganisha na masoko. Tayari Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI imetoa maelekezo kwa Halmashauri zote kutenga maeneo ya kilimo kwa ajili ya uzalishaji ikiwemo makundi maalum ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu”Alisema Mavunde

Akisisitiza umuhimu wa Kongamano hilo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Foundation for Development Hope (FDH), Bw. Michael Salali alieleza kuwa changamoto kubwa inayowakumba watu wenye ulemavu na kupelekea unyanyapaa mkubwa ni umaskini. Hivyo, kongamano hilo ni muhimu sana katika kuwezesha watu wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi kwa kuzalisha bidhaa za kilimo.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Mahusiano ya Umma wa Kampuni ya Serengeti, Bw. John Wanyancha alieleza kuwa lengo la mafunzo haya ni kuwasaidia watu wenye ulemavu kuzalisha mazao ya nafaka kwa tija ili kujikimu kimaisha na kuongeza kipato chao. Vilevile, Wayancha aliongeza kuwa pamoja na kuwawezesha kuzalisha kwa tija, wataingia kwenye mikataba ya kununua mazao yote watakayozalisha kwa bei ya soko, na hivyo kuwapa fursa ya kuwa na soko la uhakika.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, ambaye ni Afisa Kilimo wa Jiji, Bi. Yustina Munishi alieleza kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wanaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa makundi maalum wakiwemo walemavu kwa kuwawezesha mikopo ambayo inatokana na asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri ili waweze kuendeleza shughuli zao za kiuchumi na kujipatia kipato.
 
Share To:

Post A Comment: