Raisa Said Bumbuli

HALMASHAURI ya Bumbuli mkoani Tanga inatarajia kuchanja chanjo ya ugonjwa wa polio watoto 29,936 wenye umri chini ya miaka mitano, ikiwa ni Awamu ya Pili ya chanjo hiyo baada ya Awamu ya Kwanza kuchanja chanjo hiyo kwa watoto 29,013.


Hayo yalisemwa na Mratibu wa Huduma za Chanjo Msaidizi wa Halmashauri ya Bumbuli Kulwa Sadiki kwenye kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi (PHC) kwenye halmashauri hiyo.


Kulwa alisema Awamu ya Kwanza iliyofanyika Mei 18 hadi 21, mwaka huu, walitarajia kuchanja watoto wa umri huo 26,466, lakini baada ya zoezi kumalizika, walichanja watoto 29,013, hivyo kuongeza idadi ya watoto watakaopata chanjo kufikia 29,936 kwenye zoezi litakalofanyika kwa siku nne (4) Septemba Mosi hadi 4, 2022.


"Zoezi la chanjo la ugonjwa wa polio kwa Awamu ya Kwanza, tulifanikiwa kwa kiasi kikubwa. Makadirio yetu ilikuwa kuchanja watoto 26,466, lakini tuliweza kuchanja watoto 29,013. Hivyo malengo yetu sasa ni kuchanja watoto 29,936.


"Na tunatarajia kuwafikia watoto waliopo kwenye vijiji vyote 83 vya Halmashauri ya Bumbuli vilivyopo kwenye kata 18 katika tarafa tatu za Bumbuli, Mgwashi na Soni" alisema Sadiki.


Akizungumza na Wajumbe wa kikao hicho, Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Bumbuli Dkt. Charles Zawagholi alisema wamejipanga kufanikisha zoezi hilo, ambapo baada ya wahisani kutoa mafuta, wameiomba halnashauri kutoa magari tisa.


Hivyo wanatarajia kutumia magari tisa na pikipiki nne kwa maeneo ambayo yatafikiwa kwa urahisi kwa kutumia pikipiki, na hiyo ni lutokana na jiografia ya halmashauri hiyo. Pia  ili kufanikisha, watatumia matangazo kwa kutumia gari, viongozi wa dini kutangaza misikitini na kanisani, na viongozi wa vijiji ngazi zote kuanzia vitongoji, vijiji na kata.


"Tunataka hili zoezi letu tulifanye kwa weledi mkubwa ili kuona halmashauri yetu inafanya vizuri kitaifa. Hivyo viongozi wa dini mliopo kwenye Kamati hii ya PHC, tunaomba muende mkawaeleze viongozi wa dini wawatangazie waumini wao. Pia viongozi wa vijiji waweze kuweka matangazo kuanzia ofisi za vijiji na kila kona ya vijiji vyao" alisema Dkt. Zawagholi.


Mwenyekiti mpya wa Kamati ya Huduma za Jamii (Elimu, Afya na Maji) wa Halmashauri ya Bumbuli, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mahezangulu Rashid Sebarua, alisema anajua halmashauri yake ina magari machache, lakini ni muhimu ikatafuta magari hayo tisa ili kufanikisha zoezi hilo.


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bumbuli Mhandisi Olais  Sikoi alisema atahakikisha magari hayo yanapatikana ili kuona wataalamu na watendaji wanakwenda kwenye vijiji vyote 83 kuchanja chanjo hiyo.

Share To:

Post A Comment: