Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb) amezindua Kamati ya wataalamu watakaofanya utafiti fuatilizi  "tracer Study" wa wahitimu wa mafunzo ya ufundi kutoka Vyuo vya Ufundi Stadi  nchini ili kubaini ubora, ujuzi na uwezo wao kulingana na mahitaji ya soko kwa lengo la kuboresha mfunzo hayo.  


Kamati hiyo inaongozwa na Dkt. Hamisi Mwinyimvua kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wajumbe wengine ambao ni Prof. Deogratius Mushi (UDSM), Dkt. John Chegere (UDSM), Dkt Claude Maeda (SUA) na Dkt  Ibrahim Kadigi (SUA).


Akizungumza Jijini Dodoma mara baada ya kuzindua Kamati hiyo, Waziri Mkenda amesema kwa sasa msukumo  mkubwa uko katika masuala ya ujuzi hivyo taarifa itakayotokana na utafiti huo itakuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha elimu inayotolewa inatoa ujuzi utakaowezesha wahitimu kuwa na ujuzi utaokawezesha kuajiriwa ama kujiajiri.


“Tunafanya ufuatiliaji ili tutakapopitia mitaala ya mafunzo ya Ufundi Stadi tujue tunakwenda vipi kwa kuwa tutakuwa tumefahamu mahitaji ya soko na tunakoenda tunataka wahitimu hawa wakimbiliwe na waajiri ” amesema Prof. Mkenda.


Waziri Mkenda ametumia nafasi hiyo kuwataka wale wote watakaohusika katika utafiti huo kutoa ushirikiano kwa kuwa lengo ni kuboresha na kufikia malengo makubwa ya Taifa ambayo ni kutoa elimu yenye ujuzi.


Kwa upande wake Kiongozi wa Kamati hiyo Dkt. Hamis Mwinyimvua amesema utafiti utakaofanyika utahusisha wahitimu wa VET wa kuanzia mwaka 2017 hadi 2021 waliopata elimu hiyo kupitia mifumo mbalimbali ya mafunzo hayo.


Amesema utafiti huo utafanyika nchi nzima na utahusisha wahitimu wa vyuo mbalimbali vya Serikali na binafsi, waajiri walioajiri wahitimu wa VET na wale ambao hawaja ajiri wahitimu hao, walimu na wakufunzi wa vyuo hivyo, Mabaraza ya Kisekta, Chama cha Waajiri nchini (ATE) , Shirkisho la Sekta Binafsi (TPSF) na wadau wengine.


Amesema baadhi ya maeneo watakayoangalia katika utafiti huo ni iwapo wahitimu hao wameajiriwa, namna wanavyotumia utaalamu wao katika kazi wanazotekeleza, changamoto na kama ujuzi walioupata unaendana na soko la ajira. 


“Kwa ujumla utafiti unalenga kutathmini athari chanya au hasi za muda mrefu kwa programu mbalimbali za elimu ya ufundi stadi ili kupata taarifa zitakazo wezesha kuboresha mitaala na mazingira ya utoaji elimu na mafunzo hayo pamoja na kubaini changamoto za wahitimu hao  kwenye soko la ajira,”  amefafanua Dkt. Mwinyimvua.


Share To:

Post A Comment: