Moses Mashalla,


Waziri wa Maji nchini,Jumaa Aweso jana “aligeuka mbogo “ baada ya kulazimika kuchukua simu yake ya mkononi na kuwapigia baadhi ya wakurugenzi wa mamlaka za maji na kuwauliza wanatoza kiasi gani bei ya uniti moja ya maji.


Hatua hiyo inafuatia baada ya kukuta Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Karatu (KARUWASA) na Mamlaka ya Utoaji wa Huduma ya Maji Vijijini (KAVIWASU) wilayani Karatu zikitoza bei ya uniti moja ya maji kuanzia 3,000 mpaka 3,500.


Awali waziri kabla hajanyanyua simu yake ya mkononi aliwasimamisha wakurugenzi wa Mamlaka wa mamlaka hizo za maji wilayani Karatu na kuwataka wampatie maelezo ya kina kuhusu bei hizo na vyanzo vyao Maji na baadae akawauliza ni wapi waliyapata hayo mamlaka ya kutoza bei hiyo.


“Kwa lugha nyepesi hapa kuna mgongano bei za mfukoni anayeumia ni mwananchi wa kawaida naomba kujua ni wapi mmepata mamlaka ya kutoza bei hizi?”alihoji Aweso 


Hatahivyo,ghafla alivyomaliza kuwahoji wakurugenzi hao alimuamuru katibu wake,Gipson George kumpatia simu yake ya mkononi haraka na kisha kuanza kuwapigia simu baadhi ya wakurugenzi wa mamlaka za maji nchini na kuwauliza wanatoza kiasi gani bei ya uniti moja ya maji.


Waziri Aweso alimsimamisha mkurugenzi wa mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mkoani Arusha (AUWSA),Mhandisi Justine Rujomba na kumuuliza anatoza kiasi gani na ndipo Rujomba aliposimama na kufafanua wao wanatoza sh 1,350 kwa uniti moja.


Hatahivyo,Aweso hakurudhika na kumpigia simu mkurugenzi wa mamlaka ya Maji mkoani Kilimanjaro ambapo alisema wao wanatoza 1,800 na kisha kumpigia simu mkurugenzi wa maji wilayani Babati aliyetamka hadharani wao wanatoza sh 1,800.


Mara baada ya kumaliza kupiga simu hiyo waziri Aweso aliamuru bei ya uniti moja ya maji inayostahili kutozwa wilayani Karatu kuanzia sasa ni sh 1,300 kitendo kilichoibua shangwe kikaoni hapo.


Mbali na kutoa agizo hilo waziri Aweso alitoa maelekezo ya kuungana kwa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Karatu (KARUWASA) na Mamlaka ya Utoaji wa huduma ya Maji Vijijini (KAVIWASU) na kutengeneza chombo kimoja kitakachotoa huduma ya Maji kwa maslahi ya wananchi wa Karatu.


Akizungumzia maamuzi hayo katika kikao hicho Sheikh Mkuu wa wilaya ya Karatu,Rajab Ally alisema kwamba wanashukuru kwa maamuzi yaliyofanywa kwa kuwa bei za awali ziliibua kero na mateso kwa wakazi wa wilaya hiyo.


Naye diwani wa kata ya Magugu,Eltumaini Rweyemamu alisema uamuzi uliofanywa na waziri ni mzuri lakini alishauri serikali kuangalia muundo wa namna gani vyombo hivyo viwili vya Maji vitakwenda kufanya kazi.


Mwenyekiti wa halmashauri ya Karatu,Elia Morata alisema wao kama wadau hawawezi kubeza kazi iliyofanywa na KAVIWASU na kuishauri serikali itoe elimu ya kutosha kwa wananchi ni namna gani vyombo hivyo vitakwenda kuwahudumia wakazi wa Karatu kwa umoja.

Share To:

Post A Comment: