Na Christina Thomas, MorogoroMKURUGENZI wa Taasisi isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na masuala ya kutoa huduma za Saratani ya Matiti Tanzania ya (TBCF) Sharon Kuzilwa amewataka wanawake kujitokeza kupata mapema vipimo na matibabu ya saratani ya mlango wa shingo ya kizazi ili kuweza kupona kabisa


Kuzilwa alisema hayo wakati wa ufunguzi wa huduma ya upimaji na matibabu ya awali ya magonjwa ya saratani ya matiti, shingo ya kizazi na tezi dume inayotolewa bure na Asasi isiyokuwa ya kiserikali ya (TBCF) kwa ufadhili wa Songas inayofanyika katika kituo cha afya cha Sabasaba Manispaa ya Morogoro


Alisema kutokana na ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi kwa sasa kuonekana kuwa ndio ugonjwa unaoongoza kwa kuchukua maisha ya kinamama kwenye masuala ya kansa kwa sasa ni vema wanawake wanajitokeza kupima na kujitambua mapema.


Aidha alizitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni pamoja na mama aliyekoma uzazi kurudia kuingia kwenye siku zake, kutokwa majimaji yenye harufu isiyo ya kawaida na maumivu yasiyo ya kawaida.


Hivyo aliwaasa wanawake wanapoona dalili hizo kuwahi vituo vya afya mapema kupima na kama wakibainika kuwa na tatizo katika hatua ya kwanza au ya pili wataweza  kuokoa maisha yao.


Naye Khasimu Chande mkazi wa Dar es salaam alisema amefanikiwa kupona ugonjwa wa tezi dume uliomsumbua tangu mwaka 2016 baada ya kupima mapema na kupata matibabu hospitalini.


Hivyo aliwashauri wanaume kujenga tabia ya kupima mapema wanapofikisha umri wa kuanzia miaka 40 na kuendelea ili wakibainika waweze kupata matibabu mapema na kupona.


MWISHO

Share To:

JUSLINE

Post A Comment: