Meneja wa TPC Mkoa wa Singida, Michael Mwanachuo.

 

 

Na Thobias Mwanakatwe, Singida

 

SHIRIKA la Posta Tanzania (TPC)  limeingia mkataba na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ili kuwarahisishia wanaoomba waweze kufanikiwa kupata mikopo kwa urahisi bila usumbufu baada ya kujaza nyaraka zote muhimu zinazotakiwa.

Posta pia imeanza kutoa huduma kwa wananchi wanaohitaji vyeti vya kuzaliwa ambapo kazi ya kujaza fomu na nyaraka zote inafanyika posta na mwananchi akikamilisha taratibu zote anakwenda kwa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kuchukua cheti tu.

Meneja wa TPC Mkoa wa Singida, Michael Mwanachuo, akizungumza na waandishi wa habari jana alisema shirika hilo limeanza kutoa huduma hizo ili kurahisisha na kupunguza usumbufu kwa wananchi.

Alisema wanafunzi wanaohitaji mikopo wanakwenda Posta kujaza fomu ambapo wapo wataalam wa kutosha wa kuwasaidia na baada ya kukamilisha zoezi la kujaza fomu zinasafirishwa kwa njia ya EMS kupeleka HESLB.

"Hivi sasa tatizo la wanafunzi kukosa mikopo kwa sababu ya kukoseakosea halitakuwepo, mhusika atakuja Posta atasaidiwa namna ya kujaza fomu zake kwa usahihi kabisa," alisema.

Kuhusu vyeti vya kuzaliwa, Mwanachuo alisema shirika limeanza kusaidia kutoa huduma hiyo ambapo waombaji wanajaza fomu kwa njia ya mtandao ambapo Posta inawasaidi na taratibu zote zikikamilika wanakwenda RITA kuchukua vyeti vyao.

Meneja huyo aliwaalika wananchi na wanafunzi kufika Posta kupata huduma hizo ambazo zinatolewa kwa haraka na kwa ufanisi zaidi ili kuliunga mkono shirika hilo.

Hivi karibuni serikali kupitia kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ilisema taasisi zote za kiserikali zitaanza kutoa huduma zote ndani ya ofisi moja.

Mpango huo ni mkakati wa muda mrefu wa serikali katika kuziunganisha taasisi za kiserikali kufanya kazi kwenye ofisi moja.

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia imeweka mikakati katika kusimamia mifumo ya kidigitali ili kupunguza usumbufu kwa wananchi pindi wanapotaka huduma kwa uharaka zaidi.


Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: