Na,Jusline Marco;Arusha

Vijana wamehimizwa kushiriki shughuli mbalimbali za kimaendeleo katika kuelekea maadhimisho ya siku ya Vijana Duniani kkiwa ni pamoja na kuisaidia jamii inayowazunguka.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya viongozi kutoka katika mashirika mbalimbali yaliyoshirikiana na Halmashauri ya Meru wakati walipotembelea Kituo cha Afya cha Leganga na kutoa msaada kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo na kufanya usafi wamamesema kuwa juhudi hizo ni katika kuhimiza vijana kujikita katika kushiriki kazi za kijamii.Afisa uwezeshaji vijana kitoka katika Shirika la SOS Chirldren Village Arusha Ndg,Philipo Bruno Namanga,katika zoezi hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari amewataka vijana kuwa mstari wa mbele katika kushiriki kazi za kijamii.

Aidha amesema kuwa katika kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais wa awamu ya sita Mhe.Samia Suluhu Hassan za kuwekeza kwa vijana,kama shirika wameendelea kubuni za miradi mbalimbali ambayo ina tija kwa vijana.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Vision of Youth Tanzania,Vicent Ulega ambaye pia ni mratibu wa shughuli hiyo amesema katika kuelekea maadhimisho ya siku ya vijana kumefanyika zoezi la usafi katika kituo cha Afya cha Leganga na utoaji wa msaada kwa wagonjwa pamoja na bonanza la vijana.

Ulega ameongeza kuwa katika siku ya kilele cha maadhimisho ya vijana kutatanguliwa na mdahalo kutoka kwa vijana mbalimbali lengo likiwa ni kujifunza na kupata taarifa za mambo mbalimbali yahusuyo maendeleo.Kwa upande wake Afisa maendeleo ya jamii kutoka Halmashauri ya Meru,Regina Tilya akizingumza kwa niaba ya mkuu wa Idara ya Maendeleo ya jamii katika halmashauri hiyo amewataka vijana kuwa na muamko wa kufanya shughuli za kijamii bila kutegemea msukumo wa mashirika au serikali.

Bi.Regina ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwahimiza vijana kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii na wasitegemee kujifunza wakiwa shuleni au vyuoni,sambamba na kuwafundisha maadili mema ili waweze kutengeneza taifa lililo na maadili mazuri.

Ameongeza kuwa mmomonyoko wa maadili kwa vijana kunatokana na malezi mabaya ambapo amewataka wazazi na walezi kuwa mstari wa mbele katika kuwalea vijana wao na kuisihi jamii kusimama kwenye nafasi yao katika kukemea na kuonya pindi watakapoona mienendo mibovu kwa vijana.

Katika hatua nyingine Peter Ndiyogi Mkazi wa Kijiji cha Kimnyaki Kata ya Kimnyaki Wilayani Arumeru ambaye ni mnufaika wa Shirika la SOS  amesema baada ya kupata fursa ya elimu ya kilimo na ujasiriamali aliiweka katika matendo kwa kujishughulisha na kilimo pamoja na ufugaji ambavyo vyote kwa pamoja vinamuingizia kipato na kuweza kuwatunza wadogo zake ambao aliachiwa na wazazi wake wakiwa wadogo baada ya kufariki.

Ndiyogi ameeleza kuwa baada ya kuanza kujishughulisha na kilimo pamoja na ufugaji hakuishia hapo bali alikusanya vijana wengi na kuanzisha kikundi cha kuweka na kukopa na kuanzisha mradi wa mashine ya kusaga na kukoboa nafaka ambayo ilimuwezesha kwa sasa kununua usafiri wake wa pikipiki.

"Sikuweza kuishia hapo,kwa kuwa nilikuwa najishughulisha na kilimo niliamua kuandika tena barua SOS kuwaomba msaada wa kuchimbiwa kisima cha maji na hawakusita walikuja na kunichimbia kisima ambacho nilichangia kiasi kidogo cha fedha na sasa nina uhakika wa kilimo changu muda wote kwasababu maji ninayo."alisema Ndiyogi

Sambamba na hayo Ndiyogi amewataka vijana wenzake kujikita na kukituma katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo ili kuweza kutimiza malengo yao kimaisha.

Share To:

JUSLINE

Post A Comment: