Na John Walter-Manyara

Serikali ya Tanzania imetoa wanyamapori 20 aina ya Nyumbu kwa jamii ya Wahadzabe ikiwa ni sehemu ya takwa lao ili wawe tayari kushiriki zoezi la Sensa  linaloanza usiku wa kuamkia Agosti 23 hadi Agosti 31 mwaka huu.

Sensa ya mwaka huu inafanyika kwa mara ya sita ambapo hufanyika kila baada ya miaka kumi.

Jamii ya Wahadzabe ni miongoni mwa makabila machache nchini Tanzania yanayoendeleza mila na desturi wakiishi Zaidi kwa kutumia uwindaji na kuokota matunda ambapo katika matukio muhimu ya serikali hulazimika kutumia mbinu mbadala ili kuweza kuwaweka pamoja na kuhudumiwa.

Mkuu wa mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere akikabidhi nyama hiyo kwa Wahadzabe katika kijiji cha Mongowa Mono amesema serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kupata idadi kamili ya wananchi wote katika maeneo yote nchini ili kuweza kupeleka huduma za kijamii kulingana na idadi ya watu.

Hata hivyo jamii hiyo ya wawindaji licha ya kuishukuru serikali kwa kuwapatia nyama hiyo,wameiomba serikali iwapatie ndege aina ya Mbuni kwa madai kuwa wanatumia Manyoya yake kwa ajili ya dawa na matambiko yao.

Kwa kuonyesha kufurahishwa kwao,Wahadzabe hao wamempa zawadi ya asali lita 20 mkuu wa mkoa wa Manyara Makongoro Nyerere na lita 10 mkuu wa wilaya ya Mbulu Sezaria Makotha.

Share To:

Post A Comment: