Kituo cha Umahiri cha Kilimo Sayansi ya Chakula na Usalama wa Lishe ( CREATES – FNS) kilichopo katika  Taasisi ya Afrika Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela kimekuwa mstari wa mbele katika kutimiza mpango wa Ushirikiano  baina ya Serikali na Sekta binafsi (PPP) kwa kuzalisha bidhaa ambazo zimesaidia kutatua changamoto za jamii.


Akizungumza na wananchi waliotembelea banda la Taasisi ya Nelson Mandela katika maonyesho ya 28 ya nanenane Themi  Jijini Arusha,  Meneja wa CREATES-FNS Bi. Rose Mosha  ameeleza kuwa mojawapo ya bidhaa iliyozalishwa na kituo kwa kushirikisha sekta binafsi ni Dawa ya NUSA iliyotengenezwa na miti dawa ya asili ambayo ni kinga  dhidi ya homa kali ya mfumo wa upumuaji, ugonjwa wa pumu, kuondoa nyama za puani na kuongeza kinga mwilini katika kupambana na magonjwa ambayo imesajiliwa na Baraza la Tiba Asili Tanzania. 




Bi. Rose anazidi kueleza  kuwa bidhaa nyingine ni Buheri wa Afya ambayo ni dawa  iliyotengenezwa na miti dawa asili inayoondoa homa kali ya mfumo wa upumuaji unaosababishwa na virusi na kuongeza mfumo wa kinga mwilini pamoja na kurekebisha magoinjwa ya moyo na kisukari.


“Dawa hizi  zimezalishwa kwa ushirikiano wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela kwa kushirikiana na Tanzania Healthy Laboratory Service Solutions Organization kupitia mpango shirikishi baina ya serikali na sekta binafsi” amesema Bi. Rose Mosha

Naye Simprosa Ngawa mmoja wa wananchi waliotembelea banda hilo ametoa pongezi  kwa kituo cha CREATES-FNS  pamoja na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela kwa kuwa mstari wa mbele kutoa bunifu ambazo zinatatua changamoto  zinazoikabili jamii.


Share To:

Post A Comment: