Na John Walter-Babati

Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini Paulina Gekul amewakabidhi viongozi mbalimbali wa chama cha Mapinduzi jimboni hapo Mitungi ya gesi ikiwa ni jitihada za kuhimiza matumizi ya nishati Mbadala.

Gekul amekabidhi mitungi 500 leo agosti 17,2022 kwa viongozi hao wa chama hicho  kuanzia ngazi ya mashina hadi mkoa.

Akizungumza wakati akikabidhi Mitungi hiyo,Gekul amewataka viongozi wa mitaa,kata na wilaya wakahamasishe wananchi juu ya utunzaji wa Mazingira na kuacha tabia ya kukata miti ovyo kwa matumizi ya kuni na mkaa kwa kuwa inapelekea ukame na matokeo yake ni ukosefu wa mvua.

Amesema lengo la serikali ya awamu ya sita chini ya Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wananchi wanaachana na matumizi ya mkaa na kuni na kutumia nishati ya gesi ili kuepuka mabadiliko ya tabia nchi.

Aidha amesema mitungi hiyo aliyoitoa kwa ajili ya viongozi hao kuanzia mabalozi sio kwa ajili ya kampeni ya kitu chochote kwa kuwa kwa sasa hagombei nafasi yoyote na hafanyi siasa.

"Sifanyi siasa,sigombei chochote ila nafanya haya kama mbunge kuwapatia wananchi wangu nachoona naweza,naomba nieleweke hivyo" alisema Gekul

Ameongeza kuwa alikutana na mkurugunzi wa kampuni ya ORYX ENERGIES ambapo alimueleza kuhusu mpango wake wa kuhakikisha Jimbo la Babati mjini linaachana na matumizi ya mkaa na kuni ili kuweka mazingira salama ambapo alimuahidi kumsaidia mitungi hiyo na amefanya hivyo.

Mwakilishi wa kampuni ya nishati Mbadala ya ORYX Alex Wambi amesema wanaendelea kuiunga mkono serikali kwa kusambaza gesi maeneo yote ya mjini na vijijini ambapo kwa sasa wana kampeni ya kijiji kwa kijiji.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mjini Babati Elizabeth Malley amepongeza hatua hiyo ya Mbunge kutoa mitungi hiyo ya gesi kutoka kampuni ya ORYX ENERGIES kwa kuwa itapunguza idadi ya watumia kuni na mkaa hivyo kuendeleza utunzaji wa Mazingira.


Share To:

Post A Comment: