Viongozi na wadau wa maendeleo mkoani Kilimanjaro wameipongeza serikali kwa jitihada za dhati katika  kuhakikisha mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe unakamilika. Pongezi hizo zimetolewa  wakati wa ziara ya kikazi katika mradi huo iliyofanywa  na Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb).


Viongozi hao wa mkoa wa Kilimanjaro wamesema mradi huo umechelewa  lakini sasa matumaini wanayaona kutokana na hatua zilizochukuliwa na serikali inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


“Mhe. Naibu Waziri nimetembelea mradi huu mara kadhaa lakini sikuwa nimepata mwanga wa  kutosha kuhusu utekelezaji,kwa mfano nimepita kwenye hilo eneo linalotarajiwa kusimikwa pampu lakini sikuwahi kuoneshwa hizo pampu tatu zilizoletwa,Kwa kweli niwapongeze sana kwa jitihada hizi kubwa zinazoendelea."alisema Mbunge wa Jimbo la Mwanga Joseph Tadayo.


Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mwanga Jaffary Kandege  amesema matumaini ni makubwa kwa wananchi wa Mwanga na kwamba hali halisi waliyoiona inatoa  matumaini kwamba uwezekano wa kukamilisha mradi huo kwa haraka ni mkubwa. Niwapongeze serikali yetu ya CCM. 


Aidha, Mkurugenzi wa Kampuni ya M.A Kharafi & Sons ambaye ni mkandarasi  amesema matumaini yao kwa sasa ni makubwa kutokana na nia ya dhati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutatua changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikiwakumba katika utekelezaji.  Amewahakikishia wakazi na wananchi wote  wa Mwanga kuwa wasiwe na mashaka kwani vifaa muhimu kwa ajili ya kukamilisha mradi huo vimeshawasili na baadhi ambavyo havijafika wanatarajia kuvipokea bandarini mapema.


Naye Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi amewataka viongozi wa Chama na Serikali kuhakikisha wanawapa wananchi taarifa sahihi kuhusiana na utekelezaji wa mradi huo.


"kuna watu ambao wanatoa taarifa zisizo sahihi kuhusiana na mradi huu hivyo si vema viongozi wakakaa kimya, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anatambua changamoto wanazopitia wananchi wa Same Mwanga na Korogwe na kwamba anafanya kila jitihada kuhakikisha mradi huo unakamilika." Alisisitiza Mahundi

Share To:

Post A Comment: