Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Eliamani Sedoyeka amesema matumizi ya teknolojia yataimarisha, kurahisisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi katika shughuli za uhifadhi.

Prof. Sedoyeka ameyasema hayo, leo Agosti 22, 2022 wakati akizungumza na Menejimenti na watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), wakati wa ziara yake ya kikazi katika Makao Makuu ya TAWA yaliyopo Mkoani Morogoro.

“Tuendelee kujikita kwenye masuala ya teknolojia hususani katika kutekeleza majukumu ya doria ikiwemo kuongeza vifaa vya kisasa vya ufuatiliaji kama matumizi ya satelaiti (satellite) na ndege zisizo na rubani (drones)”, amesema.

Sambamba na hilo, Prof. Sedoyeka ameipongeza TAWA kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake vizuri.

” Jukumu mlilopewa na nchi ni kubwa , mmepewa sehemu kubwa sana ya nchi, pamoja na umri mdogo wa Taasisi yenu tayari mmeonesha mafanikio makubwa ya kuyatunza maeneo mnayoyasimamia, kazi mnayofanya ni ngumu na nyeti na sisi kama viongozi tunaitambua na kuithamini sana” amesema Prof. Sedoyeka.

Vilevile, Prof. Sedoyeka amewataka watumishi wote wa TAWA kuendelea kuwa wabunifu ili kuongeza tija katika Taasisi.

Awali, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi -TAWA aliwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa TAWA yakiwemo majukumu ya TAWA, mafanikio mbalimbali ya Taasisi yakiwemo kupungua kwa shughuli za ujangili na uboreshaji wa miundombinu ya utalii inayoendelea katika mapori wanayosimamia.

Vilevile Kamishna Mabula amemshukuru Prof. Sedoyeka kwa kutenga muda wake kuitembelea TAWA na kuahidi kutekeleza mapendekezo yote aliyoyatoa.
Share To:

Post A Comment: