Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mama Zainab Kombo Shaib, amesema mafunzo kwa wajasiriamali ni fursa muhimu ya kujiletea maendeleo na kujikwamua kiuchumi, kwa maslahi ya jamii na Taifa kwa ujumla.


Mama Zainab ambaye pia ni Mwenyekiti wa ‘NURU FOUNDATION’ ya Zanzibar, ameyasema hayo leo, katika Hafla ya Ufungaji wa Mafunzo ya Usarifu wa Matunda na Mbogamboga kwa Wajasiriamali Wanawake yaliyofanyika huko Chuo cha Karume Mbweni, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.


Amesema Serikali na wadau mbali mbali wa maendeleo wamekuwa wakitoa fursa za mafunzo kwa wajisiriamali tofauti, kwa lengo la kuungamkono jitihada za nchi na kuiwezesha jamii kupunguza ugumu wa maisha, na kwa mustakbali wa maendeleo ya wananchi wote.


Aidha amesema kwamba kuwepo kwa vituo vya ujasiriamali ni hatua kubwa ya kujikimu kimaisha kwa makundi mbali mbali nchini na hivyo kuchangia kupunguza idadi kubwa ya wananchi,  hasa rika la vijana, ambao wanategemea ajira kutoka serikalini.


Amefahamisha kwamba wajasiriamali wengi wanakabiliwa na changamoto katika uendeshaji wa shughuli zao zikiwemo uhaba wa masoko, maeneo ya kufanyia-kazi, ujuzi wa utengenezaji wa bidhaa bora zinazohimili soko la ushindani, pamoja na mitaji ya kuendesha biashara, na kwamba Serikali itajitahidi kuwaunga- mkono ili kuleta tija zaidi.


"Kinachohitajika kwasasa ni kujiunga na vikundi vilivyosajiliwa, ama kuanzisha vikundi na kuvisajili ili kuweza kupata mikopo ya gharama nafuu itakayowawezesha kufanya vyema shughuli zenu", amesisitiza Mama Zainab, huku ametoa wito kwa wahitimu hao kuzingatia elimu waliyoipata na kuitumia vyema, ili kuifaidisha jamii yote.


Naye Waziri ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Riziki Pembe Juma, amesema kuwa, jukumu la kuwawezesha wanawake ili kuweza kujitegemea, linatekelezwa na Wizara zote mbili, kupitia programu mbalimbali, zikiwemo za ushiriki wa wanawake katika uchumi, mafunzo, upatikanaji wa masoko, na utafutaji wa fursa za Mikopo yenye masharti nafuu isiyokuwa na riba.


Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wa mafunzo hayo Mwanafunzi Glory Hashim Badi, amesema baada ya kupata  mafunzo hayo, hatua inayofuata ni kutekeleza kwa vitendo dhana ya utengenezaji bidhaa za matunda na mbogamboga, pamoja na kuwashajihisha wengine kupata mafunzo ya ujasiriamali, ili kusaidia Serikali  kupunguza mzigo wa ukosefu wa ajira.


Mapema, Mama Zainab ametembelea na kukagua bidhaa za wajasiriamali hao, kabla ya kuwatunuku Vyeti vya Ushiriki wa Mafunzo hayo ya Wiki Tatu, yaliyowajumuisha washiriki 22 kutoka katika Vikundi 19 vya Uguja na Pemba, ambayo yameandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara ya Nchi Afisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, pamoja na Ufadhili wa ‘Zanzibar Technology and Business Incubator’.


Viongozi mbalimbali wamejumuika katika kikao hicho wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi Mariam Juma Saadalla, pia Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Bi Abeida Rashid Abdalla.




Kitengo cha Habari

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar

Agosti 05, 2022

Share To:

Post A Comment: