Waziri wa Kilimo Hussein M. Bashe leo amezindua kituo cha huduma kwa wakulima ambapo wakulima na wadau wa kilimo watapata huduma mbalimbali kwa kupiga simu ya bure na kupatiwa taarifa mbalimbali za mambo yahusuyo kilimo.


Kituo hicho cha Huduma(_Call Centre_) kimezinduliwa leo Dodoma kwa lengo mahususi la kuwapatia wakulima taarifa mbalimbali za kilimo pamoja na kusikiliza na kutatua kwa haraka changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima kwa kupiga namba ya 0733 800 200 bila gharama yoyote.


“Ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwamba lazima wizara iwafikie na kuwahudumia wakulima kwa ukaribu mkubwa ili kufikia malengo tuliyojiwekea katika kuikuza sekta hii muhimu ya kilimo.


Baada ya jana kuzindua mfumo wa usajili wa wakulima nchi nzima,leo ninazindua kituo cha Huduma kwa wakulima kwa lengo la kuwapatia wakulima na wadau wa kilimo taarifa muhimu kuhusiana na sekta ya kilimo.Hakutakuwa na gharama yoyote kwa mkulima kupiga simu kwa ajili ya kupata taarifa sahihi,na hivyo nitoe rai kwa wakulima kuitumia fursa hii.


Imani yetu ni kwamba kituo hichi kitarahisisha upatikanaji wa taarifa za kilimo kwa wakati na kutoa taarifa sahihi za kilimo ili wakulima wa Tanzania na wadau wa kilimo waweze kupiga hatua na kufikia malengo ya Ajenda 10/30”Alisema Bashe


Akitoa maelezo ya awali,Katibu Mkuu wa Kilimo Andrew Massawe amesema kwamba kituo hicho kitaboreshwa kwa miundombinu ya kisasa ili kiongeze ufanisi katika kuwahudumia wakulima wa Tanzania,na kwamba kwa sasa Wizara imejipanga kutumia   mfumo wa Kilimo Mtandao katika kutoa huduma stahiki kwa wakulima na wadau wa kilimo.


Akimkaribisha Waziri Bashe,Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde amebainisha mkakati mwingine mkubwa ambao unatarajiwa kutekelezwa na Wizara ambao ni uanzishwaji wa Chaneli maalum ya KILIMO kwenye Vituo vya Televisheni ili kufikisha habari za kilimo kwa umma na kwa uharaka zaidi kuendana na maendeleo ya teknolojia.







Share To:

Post A Comment: