Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, amesema kuwa matarajio makubwa ya Taifa kwa Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika Mataifa ya Kigeni, ni kuijenga zaidi Diplomasia ya Uchumi. 


Mheshimiwa Othman ameyasema hayo mapema leo, akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Indonesia, Bwana Macocha Moshe Tembele, aliyefika Ofisini kwake Migombani Jijini hapa, kwa lengo la kujitambulisha na kuagana, ili kuelekea katika Kituo chake kipya cha kazi.


Amesema matarajio hayo yanakuja kutokana na ukweli kwamba Nchi hii imekuwa na fursa kubwa za fungamano la kiuchumi na biashara, mbele ya Mataifa mbali mbali ya kigeni, tangu asili na zama.


Mheshimiwa Othman ametaja fungamano na nchi ya Indonesia kuwa ni la kipekee, kutokana na uwiano wa kihali, kijamii na kiutamaduni uliopo tangu zamani, kati ya Mataifa mawili hayo yenye mfanano wa asili na baadhi ya sera kwa kiasi fulani.


Aidha ameitaja Indonesia katika mnasaba wa uchumi wake wa biashara na hasa uzalishaji wa Zao la Karafuu na mafanikio yake makubwa, kupitia uendeshaji wa Mifumo ya Fedha (Islamic Finance) kutokana na Miongozo ya Kiislamu, kwa kutumia mbinu za kisasa, hali ambayo imeongeza tofauti na Nchi hiyo, hata ndani ya Soko la Dunia (World Market).


“Naamini tunaweza kuwa na mahusiano mazuri zaidi pamoja na Indonesia hasa kupitia fursa za kibiashara”, ameeleza Mheshimiwa Othman.


Hivyo amesema kuwa, pamoja na mikakati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kulihuisha upya zao za Karafuu hapa Nchini, ni wajibu wa Mabalozi kuitumia fursa hiyo ya Kidiplomasia katika kuitangaza zaidi Nchi, na kusambaza taarifa juu ya vivutio viliopo.


Pamoja na ushauri huo, Mheshimiwa Othman amepongeza hatua ya kuaminiwa na kupewa heshima Balozi huyo, kwa kuthamini uwezo wake wa utendaji, ili kuliwakilisha Taifa nje ya Nchi, huku akimtakia safari njema na kila la kheri, katika Kituo chake Kipya cha Kazi.


Naye Balozi Tembele ameshukuru miongozo aliyopewa, huku akiahidi kutekeleza maelekezo, yakiwemo kutumia mbinu bora kupitia Tafiti za Masoko (Marketing Research) ili kusaidia kuzijengea uwezo taasisi za hapa Nchini, sambamba na kukuza mifumo bora ya uendeshaji wa biashara.


Balozi Tembele aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushika nafasi hiyo hivi karibuni, baada ya kutumikia sehemu mbali mbali za utendaji, ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: