Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka ya udhibiti wa mkondo wa juu wa Petroli nchini (PURA) Mhandisi Charles Sangweni 


Na Moses Mashalla 

Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka ya udhibiti wa mkondo wa juu wa Petroli  (PURA),Mhandisi Charles Sangweni amesema kuwa kupatikana kwa bodi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli hapa nchini(TPDC) kutasaidia mamlaka yao kuongeza majukumu ,udhibiti na  wigo mpana katika usimamizi wa sekta hiyo.


Pia amesema kwamba anaamini kupatikana kwa bodi ya TPDC kutasaidia kuongeza  idadi ya mikataba na makampuni ya Utafiti wa mafuta nchini ambako kwa Sasa Kuna Jumla ya mikataba 11 na makampuni 8.


Mhandisi Sangweni alitoa kauli hiyo Wakati akihojiwa na waandishi wa habàri mara baada ya Waziri wa nishati nchini, January Makamba kuzindua bodi ya TPDC Jijini Arusha.


Akiongea na waandishi wa habàri Mhandisi Sangweni alisema kuwa PURA kama wathibiti wanaamini ya kwamba kupatikana kwa bodi ya TPDC kutasaidia kuongeza majukumu katika eneo la usimamizi wa mafuta.


"Tuna mikataba 11 na makampuni 8 kama TPDC itakwenda kwa kasi tunaamini idadi ya makampuni itaongezeka sisi kama wathibiti hii itatuongezea majukumu" alisema Mhandisi Sangweni 


Hatahivyo, alisema kwamba kupitia sheria ya Petroli ya Mwaka 2015 kipengere Cha 50 imempa mamlaka Waziri wa nishati kuipendelea TPDC na kuikabidhi vitalu vya mafuta kuviendesha bila kufungua zabuni  hivyo anaamini kupitia sheria hiyo Shirika hilo litatumia fursa hiyo kuongeza vitalu kadhaa.


Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPDC , James Mataragio alisema kuwa Shirika lao liko katika Mchakato wa Utafiti wa uchimbaji wa mafuta katika eneo la Eyasi -Sombele mkoani Manyara na tayari wameshachimba visima vifupi vitatu ambapo wamekusanya taarifa ya usumaku wa ramani ya kijographia  kupitia ndege  Mwaka 2015.


Mataragio, alisema kuwa taarifa katika eneo hilo zinaonyesha kuwa Kuna uwezekano mkubwa wa eneo hilo kuwa na mafuta na tayari TPDC wameshatangaza zabuni ya kuchukua taarifa za mitetemo ili kupata eneo la kuchimba mafuta.


"Huu ni Mradi wenye matumaini sana baada ya miaka miwili tutakuwa kwenye nafasi nzuri ya ugunduzi wa mafuta kama majirani wenzetu Kenya na Uganda waliopata mafuta katika eneo la  bonde la ufa" alisema Mataragio


Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini Mhandisi James Mataragio
 

Share To:

Arusha Newsroom

Post A Comment: