Balozi wa zao la Pamba nchini Aggrey Mwanri akionesha jembe la palizi kwa ajili ya zao la pamba na mazao mengine
Balozi wa zao la Pamba nchini Aggrey Mwanri akielezea kuhusu jembe la palizi kwa ajili ya zao la pamba na mazao mengine
Balozi wa zao la Pamba nchini Aggrey Mwanri akizungumza na Maafisa Mawasiliano wa Wizara ya Kilimo na Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) waliotembelea wadau wa pamba Kanda ya Ziwa, Julai 15,2022 mkoani Shinyanga.
Balozi wa zao la Pamba nchini Aggrey Mwanri akizungumza na Maafisa Mawasiliano wa Wizara ya Kilimo na Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) waliotembelea wadau wa pamba Kanda ya Ziwa, Julai 15,2022 mkoani Shinyanga.
 

 
Balozi wa zao la Pamba nchini Aggrey Mwanri ameipongeza serikali kwa namna ilivyofanya mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo kwa kuongeza bajeti ambapo bajeti hiyo italeta mabadiliko makubwa kwa wakulima.
 
Katika mwaka 2022/2023, Bajeti ya Wizara ya Kilimo imeongezeka kutoka Shilingi 294,162,071,000 hadi Shilingi 751,123,280,000 sawa na ongezeko la asilimia 155.34 225 429 ambapo Sehemu kubwa ya fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji, miundombinu ya uhifadhi wa mazao, kuimarisha upatikanaji wa masoko ya mazao, kuimarisha utafiti wa kilimo, uzalishaji wa mbegu na utoaji wa ruzuku.
 
Akizungumza na Maafisa Mawasiliano wa Wizara ya Kilimo na Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) waliotembelea wadau wa pamba Kanda ya Ziwa, Julai 15,2022 mkoani Shinyanga, Mwanri amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeonesha jitihada na mabadiliko makubwa katika kusimamia sekta ya kilimo kwa kutenga bajeti kubwa, ambayo itatoa ruzuku za pembejeo na kuendelea kutoa elimu ya kilimo chenye tija ili kubadilisha Kilimo kiwe na tija zaidi.
 
“Tuna Serikali iliyo makini ‘serious’ na inachokifanya kwenye kilimo, ni vyema vijana wakachukua fursa kwenye kilimo kwani kilimo ni biashara. Fursa hazitolewi, fursa zinachukuliwa. Wananchi waunge mkono mambo mazuri yanayofanywa na serikali kwa kufanya kazi kwa vitendo kwa kulima kwa tija ili tupate malighafi nyingi kwa ajili ya viwanda vyetu na kwa upande wa zao la pamba tutapata mafuta mengi ili kutatua changamoto ya uhaba wa mafuta nchini”,amesema.
 
“Wakulima wetu wanatakiwa kuzalisha mazao kwa ziada. Huwezi kupata maendeleo kama huzalishi vya ziada. Usilime kwa ajili ya kula tu, Kilimo cha mazao yote Tanzania sasa ni biashara, sasa hakuna zao la chakula tu. Lima kwa tija kibiashara”,ameongeza Mwanri.
 
Aidha amewataka vijana kuchangamkia fursa kwa kujiajiri katika kilimo akisisitiza kuwa ajira ya kweli ni kujiajiri katika kilimo na kwamba wananchi wakilima kibiashara maisha yao yatabadilika.
 
 
Katika hatua nyingine Mwanri amesema bei ya zao la pamba katika msimu huu inaridhisha tofauti na misimu mingine kwani wanunuzi wananunua kilo moja ya pamba zaidi ya bei elekezi ya serikali ambayo ni shilingi 1560 ambapo baadhi yao sasa wananunua zaidi ya shilingi 1600 na kuna kipindi bei ilifikia hadi shilingi 2020 kutokana na bei ya pamba kupanda katika soko la dunia.
 
Mwanri amewashauri vijana kuachana na dhana ya kwamba zao la pamba wanalima wazee.
 
“Kwenye zao la pamba vijana wapo wachache wanaoonekana sana kulima pamba ni wazee, lakini kwenye zao la pamba kuna ajira nyingi, vijana changamkieni fursa hii, kilimo ni biashara kinalipa na mwajiri mkuu ni kilimo”,amesema.
Share To:

Post A Comment: