Na John Walter-Babati

WANANCHI wa Wilaya ya Babati Mkoani Manyara wametakiwa kushiriki zoezi la sensa ya watu na makazi  linalotarajiwa kufanyika tarehe 23 Agosti mwaka huu, ili serikali iweze kutenga bajeti ya maendeleo kwa kujua idadi ya watu wake.

Hayo yamesemwa katika kijiji cha Tsamas kata ya Qash wilayani Babati na Mbunge wa Babati Vijijini Daniel Sillo alipokuwa akizungumza na wananchi akiwa katika ziara yake ya kusikiliza kero mbalimbali za wananchi wa kijiji hicho.

Ni mwendelezo wa ziara ya Mbunge Sillo jimboni kwake katika kata 25 na vijiji 102 ambapo leo Julai 28,2022 amewatembelea wananchi wa kata ya Qash kwenye vijiji vya Tsamas na Orngadida.

Sillo amesema kuwa  sensa ni suala la kitaifa ikiwa na lengo la kujua idadi ili kuweze kupata maendeleo baada ya kujuaa idadi ya wananchi.

"Sensa ni jambo muhimu kwa kujua idadi ya watu wako wangapi kwani ukishajua idadi ya watu ni rahisi kupanga bajeti ya shughuli za maendeleo,"alisema Sillo.

Halmashauri ya wilaya ya Babati ni miongoni mwa Halmashauri za mkoa wa Manyara, katika sensa iliyofanyika mwaka 2012 wilaya ya Babati Vijijini ilikuwa na watu wakazi wapatao 312,392.

Zoezi la sensa ya watu na makazi hufanyika kila baada ya miaka kumi ambapo takwimu mbalimbali hukusanywa ili kuisaidia serikali kupanga mipango yake ya maendeleo kwa kuzingatia vigezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na idadi.


Share To:

Post A Comment: