Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa Shirika  la Umeme Tanzania i (TANESCO) Mkoa wa Singida, Rehema Mwaipopo akisisitiza jambo wakati akizungumza na madereva wa bajaj na bodaboda  katika Ukumbi wa Vatican uliopo eneo la Mwenge mjini hapa juzi.
Mwenyekiti wa Chama cha Madereva na Wamiliki Pikipiki na Bajaj Tanzania (CHAMWAPITA) Mkoa wa Singida, Ahmed Mohamed, akizungumza kwenye mkutano huo. Kulia ni Diwani wa Kata ya Minga, Ibrahim Mrua.
Katibu wa Chama cha Madereva na Wamiliki Pikipiki na Bajaj Tanzania (CHAMWAPITA) Mkoa wa Singida, Abiud Mlowezi akiongoza mkutano huo.
Madereva bodaboda na Bajaj wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
Mkutano huo ukiendelea.

 

Na Dotto Mwaibale, Singida

 

SHIRIKA la Umeme Tanzania  (TANESCO) Mkoa wa Singida limewakutanisha madereva wa bajaj na,pikipiki kwa lengo la kuwaomba kuwa mabalozi wao ambao watakuwa wakitangaza huduma zinazotolewa na shirika hilo.

Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa shirika hilo Mkoa wa Singida, Rehema Mwaipopo, alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na madereva hao katika Ukumbi wa Vatican uliopo eneo la Mwenge mjini hapa.

Alisema wameamua kushirikiana na madereva hao kutokana na uwingi wao na huduma wanazozitoa ambapo kila siku wanakutana na watu jambo ambalo litasaidia kwa kiasi kikubwa kutangaza huduma za Tanesco.

Mwaipopo alisema hao watawaunganisha katika mfumo ambapo watakuwa wakipata ujumbe kwenye simu zao ambao utakuwa na taarifa mbalimbali zikiwamo za kukatika kwa huduma na umeme na wao watawajulisha wateja wanao wabeba.

Alisema pamoja na mambo mengine aliwataka madereva hao kutoa taarifa mbalimbali pale wanapoona matukio ya kuharibu miundombinu ya shirika hilo katika maeneo wanayopita.

“Kumekuwa na tabia ya watu wasio waaminifu kung’oa vyuma kwenye nguzo za umeme mkubwa kwa ajili ya kutengenezea mikokoteni ya kukokotwa na ng’ombe na matumizi mengine kama kutengeneza mapanga na zana nyingine mkiona uharibifu huo tupeni taarifa kupitia namba zetu tulizo wapa” alisema Mwaipopo.

Aidha Mwaipopo alisema msimu wa kilimo unapoanza kumekuwa na kazi ya kusafisha mashamba ambayo yapo chini ya nguzo za umeme hivyo wakati wa kazi hiyo wananchi wanatakiwa wasichome moto kwani wanaweza kusasabisha hatari hivyo aliwaomba madereva hao pindi watakapoona jambo hilo watoe taarifa.

Pia Mwaipopo aliwataka madereva hao kuwa mabalozi wa kutoa maelezo kwa watumiaji wa vyombo vya mto kutoegesha vyombo vyao chini ya nguzo za umeme na transfoma  kwani kunaweza kuhatarisha usalama wa wananchi na vyombo hivyo vya moto.

“Ninyi sasa ni mabalozi wetu jambo lolote mtakaloliona haliko sawa huko mnakoishi na kupita linalohusu sekta ya umeme tujulisheni pia kama kutakuwa hakuna matumizi ya vifaa vinavyotumia umeme kama pasi,majiko, majokofu, taa na vingine mvizime pia waambieni na wananchi wengine mnaoishi nao na wale mnaowabeba kwenye vyombo vyenu”alisema Mwaipopo.

Aidha katika mkutano huo Mwaipopo alielezea huduma mpya ya maombi ya kuunganishiwa umeme kwa njia ya mtandao iitwayo NIKONEKT i ambayo inafanyika kwa kutumia simu huku muombaji akiomba  akiwa nyumbani bila ya kufika ofisi za shirika hilo ambapo aliwaomba mabalozi hao kwenda kuielezea kwa wananchi wanaoishi nao na wale wanaowachukua katika vyombo vyao vya usafiri.

Mwenyekiti wa Chama cha Madereva na Wamiliki Pikipiki na Bajaj Tanzania (CHAMWAPITA) Mkoa wa Singida, Ahmed Mohamed alitumia nafasi hiyo kulishukuru shirika hilo kwa kufadhili mkutano na kuratibu mpango huo ambao ni muhimu kwa wananchi ambapo kama mabalozi  ameahidi watatoa ushirikiano wa hali na mali ili kufikia malengo.

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani hapa limekuja na mikakati ya kuboresha huduma zake ambapo madereva wa bajaj na pikipiki  watakuwa mabalozi wa kutangaza shughuli zinazofanywa na shirika hilo kwa wateja wao wanaowachukua.

Mikakati hiyo mipya imekuja baada ya Tanesco Mkoa wa Singida kupata Meneja mpya Mhandisi Florece Mwakasege aliyehamishiwa mkoani hapa hivi karibuni akitokea Mkoa wa Ruvuma.


Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: