Na Selemani Msuya
MKURUGENZI Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA),
Mhandisi Charles Sangweni amesema iwapo hakutakuwa na vikwazo, uzalishaji wa
Mradi wa Kuchataka Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG) katika Mkoa wa Lindi
utaanza mwaka 2025 na gesi ya kwanza itaanza kuuzwa 2030. Mhandisi Sangweni aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa
habari katika Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya 46 maarufu Sabasaba
yanayofanyika katika Kiwanja cha Mwalimu Julius Nyerere Temeke Dar es Salaam. Alisema kilichofanyika Juni 11 mwaka huu ilikuwa ni makubaliano ya awali ya
mkataba husika, kama majadiliano ya muundo wa mradi, ukubwa wa mradi, sheria
iweje na kwamba majadiliano yakikamilika wanatarajia Desemba 8 mwaka huu
watasaini mkataba uliokamilika. Sangweni ambaye ni Mwenyekiti wa Majadiliano alisema baada ya mkataba rasmi
kukamilika wanatarajia kwenda kwenye kazi ya usanifu wa mradi na namna ya
kupata fedha za utekelezaji. “Tunategemea utekelezaji wa mradi huu ujenzi wake utaanza 2025 na ndani ya
miaka minne hadi mitano utakuwa umekamilika na gesi ya kwanza itaanza kutoka
2030,” alisema. Mhandisi huyo alisema iwapo hakutakuwa na changamoto katika mradi huo
unaogharimu zaidi ya Sh.trilioni 70 utaweza kuzalisha gesi asilia kwa miaka 30.lisema katika kipindi cha ujenzi wa
mradi huo zaidi ya ajira 10,000 zitapatikana na ajira za kudumu zitakuwa zaidi
600 pamoja na kuchochea shughuli nyingine za kiuchumi kwenye eneo la mradi. Mkurugenzi huyo alisema tafiti zinaonesha kuwa utekelezaji wa miradi
mikubwa kama hiyo ikifanyika katika nchi kama Tanzania pato la taifa
litaongezeka kwa asilimia 1.5. “Huu sio mradi mdogo, wakubeza, kwani utachangia ukuaji wa uchumi kwa kasi
kubwa na pato la taifa litaongezeka kwa asilimia 1.5, ndio maana timu ya
Serikali hailali kuhakikisha mradi unatekelezwa,” alisema. Mkurugenzi huyo alisema baada ya mradi huo kuanza kuzalisha gesi asilia
wanatarajia kuuza katika nchi za Mashariki ya Mbali kama Japani, China na
nyinginezo ambazo zimeonekana kuhitaji. Aliwataka wawekezaji wa Kitanzania na wengine kujipanga vizuri katika
kutumia fursa zitakazokuwepo katika mradi huo, akitolea mfano kuwa nondo,
saruji na bidhaa nyingine zitahitajika. Mwenyekiti huyo alisema watajitahidi kuandaa mazingira wezeshi ili
Watanzania wawe kwenye viwango ambavyo vinakubalika katika miradi mikubwa kama
hiyo. Alisema wamekuwa wakkifanya mikutano na wadau mbalimbali kama wakuu wa
taasisi waweze kujiandaa kushiriki katika mradi huo ambao unaenda kuleta
mapinduzi ya kiuchumi, kijamii na maendeleo. Mkurugenzi huyo alisema azo la mradi huo lilinza mwaka 2012 ila kuna
changamoto zilizotokea, lakini kwa sasa Rais Samia Suluhu Hassan ameamua
kuendeleza na matarajio yao ni mradi kutekelezwa kwa viwango vinavyokubalika. Alisema kazi ya PURA ni kushauri Serikali kuhusu shughuli za mkondo wa
juu, kuthibiti na kusimamia Mradi wa LNG
ambao utakuwa na manufaa makubwa kwa Watanzania. Sangweni alitoa wito kwa Watanzania kutembelea banda la PURA ili waweze kupata elimu zaidi kuhusiana na mamlaka hiyo ambayo ina kazi moja ya kuhakikisha rasilimali mafuta na gesi zinagundulika na kutumika. |
Home
Unlabelled
LNG KUANZA UZALISHAJI 2030
Post A Comment: