Kufuatia uwepo wa matembezi ya kuhamasisha utalii katika hifadhi ya mlima Kilimanjaro mapema mwezi julai yanayoratibiwa na balozi wa utalii Lyidia Lukuba baadhi ya wadau wa utalii na wazee wa kimila katika eneo la Marangu wameanza kujiandaa kwa ajili ya tukio hilo la aina yake.


Mzee Gerson Mtui (71)mkazi wa Marangu Mbahe alisema ujio wa matembezi hayo licha ya kuwa unaenda kuhamasisha utalii lakini pia utaenda kuongeza fursa za kibiashara kwani kutakuwa na idadi kubwa ya watu lakini pia kuileta jamii pamoja.


"Tunapokutana watu wa aina tofauti tofauti kila mmoja anaonyesha utamaduni wake mfano sisi tumejipanga kwa ajili ya maonyesho ya chakula cha kienyeji cha Wachagga lakini pia kwa pombe ya asili na mambo mengine kibao"alisema


Gerald Lyimo ambaye ni muuza vinyago eneo la Marangu mtoni alisema kupitia matembezi hayo kutaenda kumtambulisha kwa wadau wa sanaa kwa kazi anazozifanya jambo ambalo pia litaenda kuongeza wigo wake wa ufanyaji biashara lakini pia ubunifu katika utengenezaji wa vinyago hivyo.


Bibi Nginael Maleko (78)mkazi wa Rauya alisema kuja kwa matembezi hayo kutaenda kuwaleta wakongwe katika mashindano ya kupika vyakula vya asili jambo ambalo pia linaweza kutumika kama darasa kwa ajili ya kufundisha vizazi vya sasa ambavyo vinaonekana kusahau utamaduni.


Kwa upande wake balozi wa utalii Lyidia Lukuba alisema matembezi hayo ambayo yatajulikana kama Marangu Nature Walk yataenda  kutambulisha aina mpya ya vivutio ambavyo kwa namna moja ama nyingine vinaonekana kusahaulika ambavyo vipo ndani ya hifadhi hiyo.


Alisema utalii hufanywa kwa njia mbali mbali lakini  katika matembezi hayo  yatahusisha pia mbio za baiskeli kilomita 40 na zitaenda kuanza katika geti la Marangu hadi kituo cha Mandara ndani ya hifadhi ya mlima Kilimanjaro



"Matembezi ya  kilomita 5 yatafanyika katika kivutio cha utalii cha Ndoro Walter falls na kumalizikia kwa  kwa Hosea wakati yale ya kilomita 10 yatamalizikia Kinukamori na kuwa matembezi haya yanatarajiwa kufanyika julai 10 mwaka huu ambapo mgeni rasmi atakuwa naibu waziri wa maliasaili na utalii Marry Masanja"alisema


Aliongeza kuwa  mwakani pia matembezi hayo yatafanyika japo inaweza zisiwe tarehe kama hizi lakini pindi yanapofanyika jamii huwa na muitikio chanya hivyo kuonyesha utayari wa kushiriki.

Share To:

Arusha Newsroom

Post A Comment: