Na Thobias Mwanakatwe

 

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma  mkoani Mara kimesema makundi  yanayotengenezwa na baadhi ya viongozi ndio chanzo cha kutokea malumbano yasio na tija kwenye uchaguzi unaoendelea ndani ya chama ngazi ya matawi.

Katibu wa Siasa na Uenezi Wilaya ya Musoma, Abubakari Nyamakato, alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kufuatia taarifa zilizoripotiwa kwenye vyombo vya habari kwamba Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Musoma, Magiri Benedictor anadaiwa kupigana ngumi na Katibu wa Wazazi wilaya, Zainabu David wakati wa uchaguzi wa  chama tawi la Nyasho.

Nyamakato alisema kimsingi tukio hilo halikutokea bali limepikwa na baadhi ya viongozi ambao wamekuwa vinara wa kutengeneza makundi ndani ya chama na kuwajengea chuki wengine kutokana na hofu ya kuja kuangushwa katika uchaguzi mkuu wa 2025.

"Katika Wilaya yetu hii viongozi wawili (anawataja majina) ndio wamekuwa ni tatizo na mabingwa wa kutengeneza makundi ndani ya chama na hata katika tukio hili la uchaguzi tawi la Nyasho wamehusika kutokana na maslahi yao ya kisiasa," alisema.

Nyamakato alisema kilichojitokeza ni kwamba baada ya kutokea malumbano yaliyotokana na baadhi ya wajumbe wa mkutano wa tawi kuonekana sio wakazi wa tawi la Nyasho jambo hilo lilipofika wilayani ilitolewa agizo uchaguzi katika tawi hilo uahirishwe ili kuorodhesha upya wajumbe halali wa tawi ndipo uchaguzi ufanyike.

"Kimsingi hakuna ugomvi wala kupigana Mwenyekiti na Katibu wa Wazazi kilichotokea wajumbe walikuwa wanabishana baada ya kubainika kulikuwa na wajumbe ambao sio wakazi wa tawi la Nyasho," alisema.

Aliongeza kuwa baada ya kutokea malumbano hayo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ambaye ndiye msimamizi mkuu wa chama alifika eneo hilo na kuagiza uchaguzi uahirishwe kwanza ili kuepusha vurugu zaidi zisitokee.

"Kudai kwamba Mwenyekiti wa CCM amepigana na Katibu wa Wazazi huku ni kutaka kuchafua Mwenyekiti aonekane hafai kwasababu wapo viongozi waliojipanga kutaka kumchafua ili malengo yao ya kisiasa yaweze kutimia," alisema.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Musoma, Magiri Benedictor, alisema yeye ni mkongwe katika mambo ya  siasa hivyo kamwe hawezi kufanya tukio la kupigana na Katibu wa Wazazi wilaya na kwamba kinachofanyika ni baadhi ya viongozi wasiompenda kutaka kumchafua kisiasa.

" Mimi katika uongozi wangu nimekuwa na misimamo isiyoyumba ambapo katika kukiongoza chama nazingatia kanuni na taratibu za chama sasa hilo ndilo linalowaumiza mahasimu wangu wa kisiasa na sasa wananitengenezea mizengwe kunichafua," alisema.

Benedictor alisema kama kweli alihushika kumpiga Katibu wa Wazazi suala hilo lingekuwa limefikishwa polisi lakini hadi sasa halijapelekwa kokote zaidi ya kuandikwa kwenye vyombo vya habari.

Aliongeza kuwa pamoja na mipango michafu inayofanywa na mahasimu wake wa kisiasa kumchafua haitamkatisha tamaa katika harakati zake za kukipigania chama na kukiongoza katika maadili ili kiendelee kuwa kimbilio la wananchi katika kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: