SPIKA wa Bunge Tulia Ackson akizungumza Bungeni wakati wa Timu ya wanawake ya soka chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Girls) ilipowasili bungeni



Na John Mapepele  

Timu ya wanawake ya soka chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Girls) imeweka  historia  ya kuwa  timu ya  kwanza kupewa heshima na Bunge la Jamhuri ya Muungano kuingia  na kukaa kwenye viti vya mawaziri ndani ya bunge  baada ya kufuzu kuingia  mashindano ya dunia ikiwa ni heshima ya mashujaa wa Taifa kwa kazi kubwa iliyoifanya ambapo kesho ni zamu ya Timu ya soka ya Taifa ya Walemavu ya (Tembo Warriors) ambayo pia imefuzu  mashindano ya dunia ya soka kwa walemavu.

Akiongea   mara baada ya kuketi eneo hilo rasmi la mawaziri, Waziri mwenye dhamana ya Michezo nchini. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema ushindi huo unatokana  na jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuiwezesha  timu hiyo katika kipindi chote cha  maandalizi wa  mashindano hayo.

“Namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muunganio wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan kwa kutuwezesha, kututia moyo na kutufuatilia kwa karibu sana katika kipindi chote” amefafanua Mhe. Mchengerwa.

Aidha, amesema Serikali itahakikisha inaendelea kuisaidia timu hiyo ili iweze kwenda  na kushinda kwenye mashindano hayo hatimaye kurejesha kombe hilo  la dunia na kuwataka wadau mbalimbali kushirikiana na Serikali katika kuwatia moyo  na kuwasaidia ili washinde.

Akizungumzia jinsi  timu ilivyopambana hadi kufika hapo amesema  kuwa  timu ilianza kuchabanga  Botswana magoli 11-0, ikaitandika  Burundi jumla ya magoli 6-1, na ikamalizia na kuibamiza timu ya Cameroon jumla ya magoli 5-1.

Kwa upande wa Warriors amesema iliishindilia Cameroon mabao 5-0, kabla ya kuikandamiza Senegal goli 1-0 na kuichakaza Morroco magoli 2-0.

Ameongeza kuwa dhamira ya Serikali ni kuendelea kufanya mapinduzi makubwa katika sekta za michezo na Sanaa ili kuipeleka Tanzania kimataifa ambapo amefafanua kuwa kuanzia Februari mwaka huu timu zote za taifa zinazoshiriki kwenya mashindano ya kimataifa  zimewekwa kambini na zinagharimiwa na Serikali.

Kwa upande wake Nahodha wa timu hiyo Noela Luhala alipewa heshima ya kuzungumza mbele ya Bunge tukufu ambapo amesisitiza kuwa kama ilivyo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Mhe, Mama Samia Suluhu Hassan kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Rais nchini ni ndoto za muda mrefu kwa timu hiyo kuwa ya kwanza kuingia mashindano ya Kombe la Dunia na kuwa Timu ya kwanza kulileta kombe hilo nchini.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania. Mhe Tulia Ackson ameipongeza timu hiyo kwa  niaba  ya bunge zima na kuwataka  kurejea na kombe hiyo  kwenye mashindano hayo.
Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: