Na Mwandishi wetu, DODOMA


MTANDAO wa jinsia Tanzania (TGNP,)  umekutana na wadau pamoja na Wabunge wanawake vinara wa jinsia Bungeni Dodoma na kuwapa mafunzo ya bajeti yenye mlengo wa kijinsia itakayowanufaisha wanawake na makundi yaliyoko pembezoni 

Mwezeshaji wa TGNP  Deogratius Temba amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yanaibua majadiliano chanya pamoja na kuzipatia ufumbuzi changamoto za masuala mbalimbali ya kijinsia hasa kwa kundi la wanawake, watoto na kundi la wenye ulemavu.


Akiongea jana Bungeni mara baada ya mafunzo hayo amesema TGNP imeendelea kushirikiana na makundi mbalimbali katika kujadili bajeti kila mwaka kwa mlengo wa kijinsia na kwamba  lengo ni kuwa na maendeleo endelevu yenye kujumuisha ustawi wa makundi yote na kudumisha haki za msingi za binadamu.



"TNGP tunafanya kila jitihada zenye lengo la kuboresha sekta za huduma kwa jamii, sekta ambazo kwa kiwango kikubwa zinawagusa wanawake moja kwa moja ikiwa  ni pamoja na kuboresha miundo mbinu ya huduma za afya na elimu hii yote ni kuamsha ari kwa  Serikali kutenga bajeti yenye kulenga na kuhamasisha utoaji wa bima za afya kwa gharama sawa na bure kwa wajane wenye uhitaji, wazee na wanawake na kaya masikini nchini,"amesisitiza 


Kutokana na hayo,Mwenyekiti wa Chama cha wabunge wanawake,Margaret Sitta amesema  kwa kushirikiana na Wabunge wenzake vinara wa jinsia watahakikisha mara kwa mara wanaisemea bajeti hiyo ya mlengo 

wa kijinsia hali itakayo ongeza uwekezaji katika kutoa elimu ya umuhimu na namna ya kuzuia magonjwa kwa watu wa pembezoni ili kupunguza gaharama za matibabu ya magonjwa yanayozuilika ikiwa ni pamoja na ujenzi wa uchumi shindani wa viwanda na kusisitiza kuwa maendeleo ya watu yanahitaji nguvu kazi ya afya bora.


"Tunawapongeza wenzetu wa TGNP kwakutushirikisha sisi pamoja na kinamama hawa na walipokuja hapa niliwauliza kwamba je,wawakilishi wenu wabunge wanayajua haya wamesema wanayajua kwa hiyo mimi nilikuwa nafikiri ni vizuri kushirikiana na wabunge wa maeneo yao kwasababu taarifa ya majimbo tunapeana pengine taarifa wananchi hawana lakini wabunge wa majimbo wanajua nini kinafanyika katika maeneo yao,"alisema.


Kwa upande wa sekta ya Maji,Mwenyekiti huyo wa wabunge wanawake Bungeni amesema watatumia nafasi yao kuishauri Serikali kutanua na kujazilisha  mtandao wa huduma ya maji safi na salama ikiwa ni pamoja na  kuondoa tozo za maji kwa taasisi za umma kama shule na vituo vya

huduma za afya.


"Ni jambo la kusikitisha kuona wanawake hawapati maji safi na salama,niwaombe wadau wote wa maendeleo kuendeleza sauti hii ya jamii lakini kwa kushirikiana na sisi wabunge ili kwa pamoja tuweze kuondokana na hii hali,tunatamani kuona hata vituo vya kulelea Watoto wenye changamoto na vituo vya wazee vinapewa maji bila gharama yoyote,"amesema mama Sitta.


Naye mmoja wa wawakilishi wa mafunzo hayo na mdau wa masuala ya kijinsia  kutoka Wilaya ya Kishapu,Mkoa wa Shinyanga  Neema Maige amesema anatamani kuona majadiliano yaliyofanyika kwenye mafunzo hayo yanazaa matunda kwa kuwa amechoshwa na changamoto ya uhaba wa maji  tikaka Wilaya yao.


Amesema ikiwa idara za maji za mikoa zitawezeshwa,hali ya upatikanaji wa maji kwa wajane, wazee, kwa tozo za viwango vya chini kabisa, au

hata bila tozo yoyote itawezekana.


"TGNP imetuwezesha kukutana hapa na wabunge vinara wa Jinsia ,tuna imani watatusaidi kufikisha sauti ya jamii sehemu husika,tunatamani kilio chetu kisikike ili kuondokana na changamoto za barabara mfano wa barabara ya kilomita 35 kutoka njia panda ya Kolandoto mpaka halmashauri ya wilaya ya kishapu  ni mbovu  inachangia kupanda kwa nauli,bidhaa za vyakula pamoja na usafiri kuwa mgumu,"amesema na kuongeza;


"Wakati mwingine tunapishana na magari ya wagonjwa yamepasuka matairi na kusababisha ajali kutokana na ugumu wa barabara sasa vitu vya namna hii lazima Serikali ifike mahali iangalie namna ya kutusaidia ili na sisi wanawake wa pembezoni tufurahie matunda ya maendeleo,"anasisitiza.

Naye Venace Mbena ametumia nafasi hiyo kuishauri Serikali kupitia sekta

ya Kilimo kuhakikisha inaweka mpngo wa kufanikisha

ushiriki wa wanawake na vijana katika uchumi shindanishi, huku akitoa mapendekezo kwa sekta ya kilimo kutenga rasilimali za kutosha

kuwalenga wanawake na vijana katika ufikiaji wa mikopo ya masharti au riba

nafuu.

Share To:

Post A Comment: