Mkuu wa Wilaya ya Bukombe Mhe.Saidi Nkumba akifungua mafunzo ya udhibiti Sumukuvu kwenye mazao kwa Wafanyabiashara, Wasafirishaji na Wasindikaji wa Mazao ya Mahindi, Karanga pamoja na bidhaa zake Wilaya ya Bukombe . Baadhi ya Wafanyabiashara, Wasafirishaji na Wasindikaji wa Mazao ya Mahindi, Karanga pamoja na bidhaa zake kutoka katika Wilaya ya Bukombe wakiwa katika ufunguzi wa mafunzo ya udhibiti Sumukuvu kwenye mazao hayo yaliyofanyika leo Juni 1,2022 wilayani Bukombe.

Mkuu wa Wilaya ya Bukombe Mhe.Saidi Nkumba akipata picha ya pamoja na baadhi ya Wafanyabiashara, Wasafirishaji na Wasindikaji wa Mazao ya Mahindi, Karanga pamoja na bidhaa zake kutoka katika Wilaya ya Bukombe wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya udhibiti Sumukuvu kwenye mazao hayo yaliyofanyika leo Juni 1,2022 wilayani Bukombe.

***********************

NA MWANDISHI WETU

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), limeendelea kutoa mafunzo ya Udhibiti wa Sumukuvu kwa Mazao ya Mahindi, Karanga pamoja na bidhaa zake kwa Wafanyabiashara, Wasafirishaji na Wasindikaji kutoka katika Wilaya ya Bukombe

Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Bukombe Mhe.Saidi Nkumba ameishukuru TBS kupitia Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu Tanzania- TANIPAC kwa kutoa kipaumbele katika suala la kuelimisha jamii ya Wilaya ya Bukombe juu ya usalama wa chakula hususan katika udhibiti wa sumukuvu ili kuweza kukabiliana na tatizo hilo.

"Ninapongeza sana jitihada za TBS kwa kupanga mafunzo haya yafanyike katika wilaya hii na mkakati mlionao wa kuendelea kuelimisha wananchi wa wilaya yetu ili waweze kukabiliana na uchafuzi wa sumukuvu katika mazao haya". Amesema Mhe.Nkumba.

Aidha Mhe.Nkumba amesema usalama wa chakula unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchafuzi wa sumukuvu ambayo husababisha madhara ya kiafya na hata kiuchumi.

"Sumukuvu huathiri zaidi mazao ya mahindi na karanga ambayo ni sehemu muhimu ya chakula chetu hapa nchini. Kwa sababu hiyo, sisi sote tunapaswa kuzingatia mikakati ya kukabiliana na changamoto ya sumukuvu ili vyakula vyetu viendelee kuwa salama kwa muda wote". Amesema

Pamoja na hayo amesema Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limekuwa likifanya jitihada za kulinda afya ya jamii kwa kudhibiti usalama na ubora wa bidhaa za chakula nchini ikiwa ni pamoja na mahindi, karanga na bidhaa zake.

Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: