Naibu Waziri wa Kilimo Mh. Anthony Mavunde amewataka vijana nchini kuchangamkia sekta ya kilimo kutokana na mpango wa serikali uliowekwa wa kuwashirkisha kundi kubwa la vijana katika kilimo ili kuwafanya vijana kuwa sehemu ya kuchochea maendeleo ya uchumi nchini na kuikuza sekta ya nchini kufikia ukuaji wa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.


Naibu Waziri Mavunde ameyasema hayo leo katika ukumbi wa Polisi Jamii,Jijini Dodoma wakati akizungumza na Vijana wa kike wa vyuo vikuu katika kongamano la fursa kwa mtoto wa kike lililoandaliwa na Taasisi ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma iitwayo Girls At Work(GAWO).

“Serikali ya awamu ya sita chini ya Mh Rais Samia Suluhu Hassan imekuja na programu ya kuwashirikisha vijana kwenye kilimo iitwayo Building a Better Tommorow(BBT) ambayo lengo lake kubwa ni kuongeza ushiriki wa vijana katika sekta ya kilimo sambamba na utatuzi wa changamoto ya Ajira kwa Vijana.

Huu ni wakati mzuri wa Vijana kushiriki kwenye sekta ya kilimo kwakuwa mipango na mikakati ya serikali imelenga kuifanya sekta ya kilimo rafiki zaidi kwa Vijana kwa kuweka mazingira wezeshi ikiwemo upatikanaji wa ardhi,pembejeo,mitaji na masoko ya mazao ya kilimo.

Mwaka huu tutaanza utekelezaji wa programu hii kwa majaribio katiko wilaya za Bahi na Chamwino mkoani Dodoma katika eneo la ekari 20,000 na baadaye tutaendelea katika maeneo mengine nchini”Alisema Mavunde

Akimkaribisha Mgeni Rasmi,Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya GAWO Bi. Witness Ponsian Mosha ameeleza malengo ya uanzishwaji wa Taasisi hiyo kuwa ni kulenga kumletea mtoto wa kike mapinduzi ya kifikra na kumuwezesha kiuchumi ili kufikia malengo yao,na hivyo wamekuwa wakiwafikia wasichana mbalimbali katika jamii kupitia makongamano na warsha mbalimbali kama sehemu ya mkakati wa kuwajengea uwezo.

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Bi. Happines Mgongo amewataka vijana wa kike kutokukatishwa tamaa na kuishi katika misingi ya maadili ili kufikia malengo waliyojiwekea.









Share To:

Post A Comment: