Na John Walter-Kiteto

Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2022 umeweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya tarafa ya Olbolot kinachojengwa katika kijiji cha Mwanya, Halmashauri ya wilaya ya Kiteto mkoani Manyara uliogharimu shilingi Milioni 609,886,000.00.

Mradi huo unaotarajiwa kukamilika juni 30,2022 unaotekelezwa na Serikali kupitia fedha za tozo za miamala ya simu na mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya Uviko 19.

Kituo hicho cha Afya kinatarajia kunufaisha wakazi zaidi ya 46,321 na wa tarafa jirani.

Baada ya kuweka jiwe la msingi katika Kituo hicho leo Juni 14,2022, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Sahil Geraruma alisema kuwa mradi huo ni miongoni mwa miradi mizuri yenye manufaa makubwa kwa wananchi.

 Aliwataka viongozi wa wilaya ya Kiteto kuendelea kusimamia mradi huo uweze kukamilika kwa wakati uliopangwa ili wananchi waanze kunufaika na kuepuka kutembea mwendo mrefu.

 Aidha amewasihi akina mama wajawazito na wenye watoto wadogo walio chini ya umri wa miaka 5 na jamii kwa ujumla kutumia kituo hicho cha afya hicho ipasavyo pindi kitakapokamilika kwa kuwapeleka watoto wao kliniki na kwenye chanjo ili wapate huduma za afya.

Geraruma alisema kuwa utekelezwaji wa mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya awamu ya sita wa kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa katika halmashauri zote hapa nchini ili kuwezesha wananchi kupata huduma bora za afya.

Naye Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mbaraka Alhaji Batenga  alibainisha kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia  wakazi wa eneo hilo kwa kuwapunguzia umbali wa kilomita 30 wanaotembea wananchi kufuata huduma za afya katika hospitali ya wilaya na kupunguza hatari ya vifo vya wajawazito na watoto.

Kwa upande wa Mbunge wa jimbo hilo  Edward Ole Lekaita aliishukuru serikali kwa kutoa pesa hizo kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha afya  cha Mwanya.

 

Share To:

Post A Comment: