WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku tano kuanzia leo Juni 8, 2022 hadi Juni 12, 2022 Wizara ya Kilimo iwe imeondoa pikipiki zote wizarani hapo na kuzikabidhi kwa wakurugenzi


“Hii haikubaliki, Wakurugenzi wote waandikiwe barua waje wazichukue, na wakazikabidhi kwa Maafisa Ugani, kama kuna ufungaji wa plate number utafanyika huko huko. Jumapili saa 10 jioni ziwe zimefika kwa wahusuka.”


Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Juni 8, 2022) alipokagua Ofisi za Wizara ya Kilimo zilizopo eneo la VETA, Dodoma na kukuta pikipiki zilizotolewa kwa ajili ya maafisa ugani zikiendelea kuwepo.


Aprili 4, 2022 Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alizindua ugawaji wa vitendea kazi vilivyoandaliwa na Wizara ya Kilimo kwa ajili ya Maafisa Ugani wote nchini. Vifaa ni pamoja na pikipiki.


Amesema tayari Mheshimiwa Rais Samia alishazikabidhi kwa ajili ya kupelekwa kwa maafisa ugani, hivyo kitendo cha pikipiki hizo kuendelea kubaki katika eneo hilo hakikubaliki.


Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Profesa Siza Tumbo amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba wamepokea maelezo hayo na watayafanyia kazi.

Share To:

Post A Comment: