Viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi na Wadau wa maendeleo wakiongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo Jerry Muro (kulia) wakivuta pazia kuashiria uwekaji wa jiwe la Msingi la Mradi wa ujenzi wa Ghala la Kisasa la kuhifadhi zao la Alizeti lililojengwa Kijiji cha  Mnang;ana, Kata ya Sepuka katika hafla iliyofanyika mwishoni mwa wiki wilayani humo mkoani Singida.
Uzinduzi huo ukifanyika.Kutoka kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi. Mwenyekiti wa wilaya  hiyo, Ally Mwanga,kushoto ni Diwani wa Kata ya Sepuka, Halima Ng'imba na Mwakilishi wa Shirika la Wanawake na Jinsia la Umoja wa Mataifa (UN-WOMEN), ambaye pia ni Mtaalam wa Kitengo cha kuwawezesha wanawake kiuchumi,  Lilian Mwamdanga.
Afisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika Wilaya ya Ikungi, Gurisha Msemo akiwa kwenye hafla hiyo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga akizungumza kwenye hafla hiyo.

Mwakilishi wa Shirika la Wanawake na Jinsia la Umoja wa Mataifa (UN-WOMEN), ambaye pia ni Mtaalam wa Kitengo cha kuwawezesha wanawake kiuchumi,  Lilian Mwamdanga akizungumza wakati wa hafla hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro, akisalimiana na wananchi waliofika kuhudhuria hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ghala hilo. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi.
DC Jerry Muro akisalimiana na wazee waliofika kwenye hafla hiyo.
Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya hiyo wakikagua Ghala hilo.
DC Jerry Muro akiwa na viongozi wa wilaya hiyo wakati wakikagua Ghala hilo.
Wazee wakiwa kwenye hafla hiyo.
Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ikungi, Haika Masawe akizungumza kwenye hafla hiyo.
Hafla ikiendelea.
Wakina mama wakiwa kwenye hafla hiyo.
DC Jerry Muro (Aliyevaa miwani na kuipa kamera mgongo) akizungumza na wananchi wakati wa hafla hiyo.
Hafla ikiendelea.
Muonekano wa Ghala hilo la kisasa lililojengwa Kijiji cha Mnang'ana Kata ya Sepuka Wilaya ya Ikungi Mkoa wa Singida.  


Na Dotto Mwaibale, Singida

 

MKUU wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro amewataka wakulima wilayani humo kuhifadhi mazao ili waje kuyauza kwa bei yenye tija.

Muro alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati akiweka jiwe la Msingi la Mradi wa Ghala la zao la alizeti ambalo limejengwa Kijiji cha Mnang'ana Kata ya Sepuka na Shirika la Wanawake na Jinsia la Umoja wa Mataifa (UN-WOMEN)  kwa Sh. 248,324,122 kwa Ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo la Japani (KOICA) mradi ambao unatekelezwa na Shirika la Farm Africa chini ya usimamizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.

“ Nataka mwaka huu wakulima wote wa zao la alizeti wanufaike kwa kuuza kwa bei nzuri na kuacha kurubuniwa na walanguzi (vishoka) ambao wamekuwa wakiyanunua kwa bei ya chini na kwenda kuyauza kwa bei ya juu" alisema Muro.

Muro aliishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea mradi huo ambapo pia alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wadau wa maendeleo Konica , UN-WOMEN na Farm Africa kwa kutekeleza mradi huo wa ujenzi wa ghala hilo.

Muro aliwataka wazazi kuwapeleka watoto wao shule za ufundi  VETA ili baada ya masomo waweze kupata mkopo  wa asilimia 10 unaotolewa na halmashauri waweze kukopa mashine za kuchomelea, kununua vyerehani na kufungua viwanda vidogo kama vya ushonaji wa nguo, utengenezaji wa vifaa vya chuma (welding) badala ya kuwaacha waende mjini hasa wasichana kutafuta kazi za ndani.

Alisema  Serikali imepanga kila kijiji hapa nchini kuhakikisha kinapata umeme na kuwa kwa Wilaya ya Ikungi wanataka umeme huo ufikishwe kwenye maeneo ya kimkakati akitolea mfano Kata ya Iyumbu ambayo ni maarufu kwa kilimo cha mpunga ambapo badala ya kuuza mpunga waanze kuukoboa na kuuza mchele ambao mifuko yake itawekwa lebo ya Ikungi jambo litakaloongeza thamani ya zao hilo na Serikali kupata mapato.

Muro alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi ya Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 23 miaka huu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi aliwashukuru wadau hao kwa hatua walioifikia ya kujenga Ghala hilo la kisasa na kuwashukuru wananchi wa Kata ya Sepuka na Kijiji cha Mnang'ana kwa kukubali kutoa eneo la ujenzi. 

Alisema ujenzi wa ghala hilo ulianza mwezi Novemba mwaka jana na kukamilika Machi mwaka huu na kuwa lengo la mradi huo ni kuongeza thamani ya zao la alizeti  kwa wakulima kwa umoja wao waweze kuyahifadhi wakati  wakisubiri bei yenye tija na kuwawezesha kujipatia kipato cha kujikimu kiuchumi.

Alisema mradi huo ni matokeo ya shughuli zilizotakiwa kutekelezwa kupitia Mradi wa Tuufikie Usawa wa Kijinsia kwa  kumuwezesha Mwanamke na Msichana na kutambua mahitaji ya kijamii.

Kijazi  alisema katika ghala hilo vimewekwa vifaa mbalimbali kama mzani wa kidigitali, kipima unyevu, projekta, mashine ya kudurufu na kutoa nakala,machekeche, mitungi ya kuzimia moto na samani za aina mbalimbali na kuwa lina uwezo wa kuhifadhi tani 300 au kilo 5000 za zao la alizeti.

Afisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa wilaya hiyo,  Gurisha Msemo alisema wamejipinga vilivyo kuhakikisha vipimo vitakavyotumiwa kuuza mazao ya wakulima ni vile vilivyopendekezwa na Serikali na si vinginevyo ili wakulima waweze kunufaika na kilimo.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: