Na John Walter-Babati

Mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange Juni 2,2022 amefungua  shule mpya ya sekondari ya Kololi iliyopo kata ya Maisaka mjini Babati.

Shule hiyo yenye jina la Diwani wa kata ya Maisaka ambaye pia ni mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Babati Abdulrahmani Kololi ina  jumla ya vyumba vitano vya madarasa ambapo viwili bado havijakamilika,ofisi mbili za walimu,moja imekamilika ,matundu nane ya vyoo vya wanafunzi pamoja na matundu manne ya vyoo vya walimu, mawili bado yanajengwa mawili na ofisi moja
Shule hiyo ambayo ujenzi wake unaendelea inajengwa kwa nguvu za wananchi wa kata ya Maisaka na wadau wengine wa maendeleo akiwemo Mbunge wa Jimbo la Babati mjini Paulina Gekul pamoja na mapato ya ndani ya halmashauri.
Shule ya sekondari Kololi ni mapinduzi makubwa ya kielimu ndani ya kata ya Maisaka na mitaa yake lakini pia imesaidia kupunguza umbali kwa wanafunzi ambapo hapo awali walikuwa wakilazimika kutembea kilomita 20 ili kufika shule ya sekondari Kwan'g.
Wananchi wa kata ya Maisaka wanasema wameamua kumpa heshima diwani huyo  kwa kuipa shule hiyo jina lake la Kololi kutokana na kazi ya kuwatumikia wananchi na ushirikiano anaotoa kwao katika kila jambo.
Wanafunzi wanasema kabla ya shule hiyo walikuwa wakilazimika kuamka mapema na kusubiri gari ili kuomba lifti hali iliyokuwa ikiwasababishia kuchelewa shuleni na kupewa adhabu huku madereva wengine wasio wastaarabu wakiwatongoza na kuwatupia maneno makali.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Babati Anna Fisoo amewaambia wananchi wa kata ya Maisaka kuendelea kuchangia miradi ya elimu pamoja na kutunza majengo ya Shule ya sekondari Kololi ili yaweze kudumu na kufaidisha vizazi vijavyo.
Naye diwani wa kata ya Maisaka Abdulrahmani kololi amesema kuanza kwa shule hiyo itapunguza changamoto ya wanafunzi kutembea kilometa 20 kwenda shule ya sekondari ya Kwan'g kwani ilikuwa changamoto kubwa kwao ambapo wazazi walilazimika kudamka asubuhi saa kumi na moja kuwasindikiza hadi barabarani kusubiri magari waombe lifti.
Share To:

Post A Comment: